Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenan Kihongosi, amewataka mabalozi wa mashina kutokubali kuchochewa na watu wasioishi ndani ya nchi kwa lengo la kuhatarisha amani na usalama wa Taifa.
Kihongosi amesema ni wajibu wa kila mwananchi kuilinda Tanzania na kutokubali kutumiwa na watu wenye nia ovu ya kuvuruga amani ya nchi, akisisitiza kuwa Taifa linapaswa kulindwa kwa wivu mkubwa.
Aidha, amewataka wazazi kuwaelimisha vijana wao ili wasikubali kutumika kama chombo cha wahalifu wanaolenga kulichoma Taifa, badala yake wajivunie na kuilinda nchi yao.
Akizungumza katika mkutano wa Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Asha Rose Migiro na mabalozi wa mashina wa CCM Wilaya ya Ilala uliofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Kihongosi amesema Chama Cha Mapinduzi kiko imara na kitaendelea kuwa salama, hususan jijini Dar es Salaam.
Amesema hakuna mtu, kundi wala genge lolote litakaloweza kuitisha CCM katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi waliyoiahidi wananchi.
Aidha, amewaomba wanachama na viongozi wa CCM kutambua kuwa chama kinawategemea wao katika kulinda hadhi na heshima yake, akisisitiza kuwa jukumu hilo ni la kila mwanachama.
“Tutupambana kwa kila namna kuhakikisha hakuna mtu yeyote atakayekidondosha Chama Cha Mapinduzi.
Miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa, ukiangalia sekta ya elimu, mambo makubwa yamefanyika ikiwemo elimu,” amesema Kihongosi.
Ameongeza kuwa hakuna sababu ya kuwa na hofu kwani CCM imefanya makubwa chini ya uongozi wake, na Ilani ya Chama itaendelea kutekelezwa kwa asilimia 100.
Aidha, amewataka wanachama kutosita kutoa taarifa pale wanapoona ucheleweshaji wa miradi ya maendeleo ambayo tayari imepangiwa fedha na Serikali.
“Tuliwaambia wananchi tunaenda kutekeleza Ilani ya Chama, na ifikapo mwaka 2030 wananchi wanapaswa kuuliza yale yote tuliyoahidi kama yametekelezwa,” amesema.
Kihongosi pia amesema Rais wa Chama ameongoza utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo, hivyo ni wajibu wa wanachama wote kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza miradi hiyo.
Amefafanua kuwa demokrasia ya kweli ni ile inayojali mahitaji ya msingi ya wananchi ikiwemo chakula, makazi na huduma za afya, akisisitiza kuwa CCM imeendelea kutekeleza wajibu huo.
Amesema demokrasia zinazolenga kuvuruga nchi hazipaswi kukubalika, kwani demokrasia ya kweli ni ile inayojali utu wa mwananchi na ustawi wa Taifa.
Akihitimisha, Kihongosi amewataka vijana kuendeleza tunu ya amani na utulivu ili kizazi kijacho kiweze kunufaika na matunda ya nchi.
“Sisi kama vijana tuna wajibu wa kuilinda amani na utulivu wa Taifa letu ili vizazi vijavyo vinufaike,” amesema.

