‎TAMISEMI YAKUTANA NA WADAU KUJADILI MKAKATI WA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

 

Na OWM-TAMISEMI, DODOMA

‎Katika jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kurejesha uoto wa asili, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) leo Januari 15,2026 imekutana wataalam kutoka kampuni ya kimataifa ya Sinoway Forest Technology Co. Ltd na pamoja na wadau kutoka Halmashauri mbalimbali nchini kujadili fursa za mabadiliko ya tabianchi katika ngazi ya jamii.

‎ Katika kikao hicho kilichoongozwa na Mkurugenzi wa Sera na Mipango Bw. John Cheyo, Mwenyekiti wa Sinoway Forest, Bwana Liu Tao, amewasilisha mkakati kabambe wa “Sovereign Ecological Restoration” (Mkakati wa Kitaifa wa Kurejesha Ekolojia).

‎Bwana Liu Tao alianza kwa kuonesha picha halisi ya hali ya uharibifu wa ardhi duniani, akibainisha kuwa zaidi ya hekta bilioni 2 zimeharibika. Barani Afrika, asilimia 45 ya ardhi imeathiriwa na kuenea kwa jangwa, hali inayozipunguzia Halmashauri mapato na kuongeza umaskini kwa wananchi wanaotegemea kilimo na ufugaji.

‎”Hatuwezi kuendelea kutegemea misaada pekee kurejesha mazingira yetu bali tunahitaji teknolojia inayoweza kutekelezwa kwa kiwango kikubwa na inayoweza kujilipa yenyewe,” amesema Bw. Tao.

‎Katika wasilisho hilo Bw. Tao ameonesha teknolojia ya kipekee ya “Seed-Balls” (mipira ya mbegu) ambayo imetengenezwa kwa virutubisho na polima maalum zinazohifadhi maji, zikilinda mbegu dhidi ya ukame na wadudu hadi mvua itakaponyesha.

‎Amesema Teknolojia hiyo inaruhusu upandaji wa miti na nyasi kwa kutumia ndege au droni (Aerial Broadcasting), ambapo hekta 1,000 zinaweza kupandwa kwa siku moja tu, jambo ambalo lingechukua miezi kadhaa kwa kutumia nguvu kazi ya binadamu.

‎Aidha Sinoway Forest wamependekeza mfumo wa Carbon Credits.

‎Chini ya mfumo huo, misitu na uoto utakaorejeshwa utatumika kufyonza hewa ya ukaa (carbon sequestration), na kisha halmashauri zinaweza kuuza hati hizo za kaboni kwenye soko la kimataifa.

‎ “Hii itazalisha fedha za kigeni na kusaidia maendeleo ya kijamii kama shule, zahanati, na maji katika ngazi ya kijiji bila kuongeza deni la Serikali,” amefafanua Bw. Tao.

‎Wasilisho hilo lilihitimishwa kwa wito wa kuunganisha nguvu kupitia “Dimbwi la Pamoja la Rasilimali za Kaboni” (Pan-African Carbon Asset Pool) itakayosaidia Halmashauri za Tanzania kuwa na nguvu kubwa ya majadiliano katika soko la dunia na kupunguza gharama za uthibitishaji wa miradi ya mazingira.

‎Wadau waliohudhuria kikao hicho walionyesha matumaini makubwa kuwa ushirikiano huo kati ya OWM-TAMISEMI na Sinoway Forest utakuwa mkombozi, si tu kwa mazingira, bali pia kwa uchumi wa wananchi wa vijijini ambao ndio waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabianchi.

   

Post a Comment

Previous Post Next Post