Mwandishi Wetu,
Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya maji, Wizara ya mambo ya nje ,Wakandarasi , Afisa kutoka Ubalozi wa India nchini Tanzania Rajnish Kumar na Mwakilishi wa Serikali ya India kutoka Benki ya Exim Ravi V. P. Singh imetembelea mradi wa miji 28 katika Wilaya ya Manyoni kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo.
Serikali kupitia Wizara ya Maji inatekeleza mradi wa maji wa miji 28 katika Halmashati ya wilaya ya Manyoni ,ambapo Mradi huo unahusisha Uchimbaji wa visima, Ulazaji wa bomba kuu, Ujenzi wa Mtambo wa kusukuma maji, Ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita 2,000,000 pamoja na Ulazaji wa bomba za usambazaji maji umbali wa kilomita 31.
Mradi huo kwa sasa umefika asilimia 65 ya utekelezaji wake na utanufaisha wakazi zaidi ya 64,000
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Manyoni Mary Kanumba amesema wananchi wanamatumaini makubwa na mradi huo kutokana na uzalishaji wa maji wa sasa kutokidhi mahitaji kuendana na ongezeko la watu na makazi katika mji huo.
Aidha ameiomba Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya India kukamilisha mradi huo kadiri ilivyo pangwa kwani utaondoa changamoto ya uhaba wa majisafi kwa wananchi wa wilaya ya Manyoni .
Kwa upande wake mwakilishi kutoka Benki ya Exim Ravi V. P. Singh amesema Serikali ya India kupitia Benki ya Exim haitakuwa kikwazo katika ukamilishwaji wa mradi huo kwani dhamira yao nikuona mradi huo una kamilika kwa wakati na wananchi wanapata majisafi na salama .
Naye Rajnish Kumar Afisa kutoka Ubalozi wa India nchini Tanzania amemwelekeza mkandarasi Mega Engineering and infrastructute Limited kukamilisha mradi huo mapema ifikapo Aprili,2026 tofauti na mwezi Julai kama ilivyo ainishwa kwenye Mkataba.







