Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi zawadi Rais wa Comoro Mhe. Azali Assoumani alipotembelea leo kambi ya madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali kutoka Tanzania inayofanyika katika kisiwa cha Anjouan. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) Dkt. Diwani Msemo.

Rais wa Comoro Mhe. Azali Assoumani akisalimiana na balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu alipotembelea leo Hospitali ya Hombo iliyopo kisiwani Anjouan kwaajili ya kuona kambi ya matibabu inayofanywa na madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali kutoka Tanzania. Madaktari bingwa kutoka Tanzania wanatoa huduma za matibabu katika hospitali nne zilizopo kisiwa Anjouan.
Daktari kutoka Global Medicare Tanzania Mary Kondowe akimvisha vazi la kimasai Rais wa Comoro Mhe. Azali Assoumani alipotembelea kambi ya matibabu ya magonjwa mbalimbali ya madaktari bingwa kutoka Tanzania inayofanyika katika hospitali nne zilizopo kisiwa cha Anjouan. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) Dkt. Diwani Msemo.
**********
Rais wa Comoro Mhe. Azali Assoumani amemshukuru Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza ahadi yake ya kuwaleta madaktari bingwa kutoa matibabu ya magonjwa mbalimbali kwa wananchi wa kisiwa cha Anjouan aliyoitoa Julai 6, 2025 katika maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Comoro.
Akizungumza na timu ya madaktari hao katika hospitali ya Hombo kisiwa cha Anjouan, Mhe. Rais Assoumani alisema utekelezaji wa ahadi hiyo ni ishara ya undugu na ushirikiano mzuri baina ya nchi hizo mbili.
“Hongereni madaktari kwa kazi nzuri mnayoifanya, sisi wana Comoro tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza ahadi yake ya kuwaleta ninyi hapa, tunasema asante sana ”, alisema Mhe. Rais Assoumani.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe. Saidi Yakubu alimweleza Mhe. Rais Assoumani kuwa wataalam 52 wenye taaluma 17 wameweka kambi ya matibabu kwa siku nane kisiwa cha Anjouan.
“Tunao madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Taasisi ya Kansa ya Ocean Road (ORCI) na Hospitali ya Benjamin Mkapa pamoja na ” amesema Balozi Yakobu
Mwenyekiti wa Utalii Tiba Taifa Dkt. Peter Kisenge alisema katika kambi hiyo madaktari wanaratajia kuwaona wagonjwa zaidi ya 3,000 waliojisajili na kwamba hadi kufikia jana wagonjwa 1361 wameonwa na madaktari bingwa.
