DKT. PETER KISENGE AWASAIDIA MADAKTARI WA ANJOUAN KUBORESHA UCHUNGUZI NA MATIBABU YA MOYO

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwafundisha madaktari wa hospitali ya Hombo iliyopo Kisiwa cha Anjoan  namna  ya kupata mwonekano bora wa moyo wakati wa kufanya kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi  ili kuboresha usahihi wa matokeo. Mfunzo hayo ameyatoa katika kambi maalumu ya madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali kutoka Tanzania inayofanyika kisiwani humo.

Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu akizungumza na daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbi (MNH) Vincent Tarimo wakati wa kambi maalumu ya madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali kutoka Tanzania wanaotoa huduma za matibabu katika hospitali kubwa tatu zilizopo kisiwani Anjoan.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimwelekeza daktari wa Hospitali ya Hombo iliyopo kisiwani Anjouan Misdjal Ali dawa nzuri za kuwatibu wagonjwa wenye matatizo ya shambulio la moyo wakati wa kambi maalumu ya madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali kutoa Tanzania inayofanyika katika Hospitali hiyo. Kulia ni Daktari kutoka JKCI Janeth Mmari.

Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu akizungumza na daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbi (MNH) Vincent Tarimo wakati wa kambi maalumu ya madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali kutoka Tanzania wanaotoa huduma za matibabu katika hospitali kubwa tatu zilizopo kisiwani Anjoan.


 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimwelekeza daktari wa Hospitali ya Hombo iliyopo kisiwani Anjouan Misdjal Ali dawa nzuri za kuwatibu wagonjwa wenye matatizo ya shambuli la moyo wakati wa kambi maalumu ya madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali kutoa Tanzania inayofanyika katika Hospitali hiyo.

*********

Madaktari wa Hospitali ya Hombo iliyopo katika Kisiwa cha Anjouan nchini Comoro wamepatiwa mafunzo maalumu ya jinsi ya kufanya vipimo vya moyo kwa ufanisi na kutoa matibabu kwa wagonjwa wenye matatizo makubwa ya moyo.

Mafunzo hayo yametolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba pamoja na kupandikiza vifaa visaidizi vya moyo.

Dkt. Kisenge alisema mafunzo hayo yanalenga kuongeza uwezo wa madaktari wa ndani kufanya uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo, kuyatambua mapema na kuyatibu kwa ufanisi badala ya wagonjwa kusafiri hadi nchi nyingine kufuata huduma hizo.

Alieleza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha huduma za moyo katika Hospitali ya Hombo kwa kuhakikisha madaktari wake wanafahamu matumizi ya mashine za uchunguziwa moyo  kama Echocardiogram (Echo) na Electrocardiogram (ECG) pamoja na namna ya kusoma majibu yake kwa usahihi.

“Tunataka madaktari wa Comoro waweze kutoa huduma bora za moyo katika vituo vyao, bila kulazimika kutegemea wataalamu kutoka nje mara kwa mara. Hii itapunguza gharama, kuokoa muda na kuboresha afya za wananchi wengi zaidi”,  alisema Dkt. Kisenge.

Kwa upande wao, baadhi ya madaktari wa Hospitali ya Hombo walisema wamefurahishwa kufanya kazi na Dkt. Kisenge kwani kupitia mafunzo hayo wamejifunza mambo mapya mengi, ikiwemo njia sahihi za kufanya vipimo vya Echo, kusoma matokeo yake na kutoa dawa zinazofaa kwa wagonjwa wa moyo kulingana na hali zao.

“Tumefurahi sana kushirikiana na Dkt. Kisenge. Ameongeza uelewa wetu wa jinsi ya kuchunguza wagonjwa wa moyo kwa undani na namna ya kuwasaidia wagonjwa kwa kutumia dawa sahihi. Tunamshukuru yeye na timu ya JKCI kwa kutuletea maarifa haya muhimu”, alisema Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto Daniel Oiridi.

Naye Dkt. Misdjal Ali mmoja wa madaktari waliopatiwa mafunzo hayo, alisema amejifunza mambo mengi ya kitaalamu ikiwemo jinsi yakupata mwonekano bora wa moyo wakati wa kufanya kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi  (Echocardiography) ili kuboresha usahihi wa matokeo

“Kupitia mafunzo ya Dkt. Kisenge nimeongeza uwezo wangu wa kufanya vipimo vya moyo kwa ufanisi zaidi. Sasa naweza kubaini matatizo ya moyo mapema na kusaidia wagonjwa kupata tiba sahihi kwa wakati”, alisema Dkt. Misdjal Ali.

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imekuwa ikitoa mafunzo kama hayo wakati wa kambi maalumu za matibabu ya magonjwa ya moyo inayozifanya ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kuboresha huduma za afya na kuongeza uwezo wa wataalamu wa ndani katika kutibu magonjwa ya moyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post