SIMBACHAWENE AKIRI UWEPO WA CHANGAMOTO YA UKIUKWAJI WA MAADILI IKIWEMO MGONGANO WA MASLAHI KATIKA SEKTA ZA UMMA.

 WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe George Simbachawene amesema kuwa pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali lakini bado kuna changamoto ya ukiukwaji wa maadili katika sekta mbalimbali.


Ambapo amesema changamoto hizo ni pamoja na matumizi mabaya ya madaraka, mgongano wa maslahi na ufujaji wa rasilimali za Umma ambapo Serikali inachukua hatua thabiti kuhakikisha maadili yanazingatiwa.

Waziri Simbachawene ameyasema hayo mapema Leo Jijini Dodoma Machi 6,2025 wakati akizungumza katika Hafla ya Uzinduzi wa Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Ofisi ya Rais,Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Chuo cha Uhasibu Arusha.

"Ndugu Washiriki, pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali, bado tunakabiliana na changamoto za ukiukwaji wa maadili katika sekta mbalimbali. Changamoto hizi ni pamoja na matumizi mabaya ya madaraka, mgongano wa maslahi, na ufujaji wa rasilimali za umma. Serikali inaendelea kuchukua hatua thabiti kuhakikisha kuwa maadili yanazingatiwa, ikiwemo kuimarisha sheria, mifumo ya uwajibikaji, na mafunzo kwa viongozi wa umma".

" Kila mmoja wetu anawajibika katika kuhakikisha kuwa maadili ya utumishi wa umma yanazingatiwa kikamilifu".

Waziri huyo pia amewataka washiriki watakaopata mafunzo haya kuhakikisha wanatumia maarifa watakayopata kwa vitendo katika maeneo yao ya kazi kwani mafunzo haya ni fursa ya kuimarisha utendaji kazi na kuleta mabadiliko chanya.

"Ninatoa wito kwa ofisi zote za Serikali kutumia kikamilifu fursa hii. Aidha, nawataka washiriki watakaopata fursa ya kushiriki mafunzo haya kuhakikisha wanatumia maarifa watakayopata kwa vitendo katika maeneo yao ya kazi. Tunaamini mafunzo haya ni fursa muhimu ya kuimarisha utendaji wao, kuleta mabadiliko chanya katika taasisi wanazoziongoza, na kuhakikisha kuwa maadili yanadumishwa kwa faida ya taifa".

Aidha ameongeza kuwa uadilifu ni nguzo muhimu ya maendeleo na viongozi wote na Watumishi wa umma wanapaswa kuwa mfano bora wa uwajibikaji,uaminifu na utendaji wa haki.

"Uadilifu katika uongozi wa umma ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa letu. Viongozi wote na watumishi wa umma wanapaswa kuwa mfano bora wa uwajibikaji, uaminifu, na utendaji wa haki. Taifa lenye viongozi waadilifu linakuwa na taasisi imara, zenye kuwahudumia wananchi kwa haki na usawa. Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa maadili ya utumishi wa umma yanazingatiwa ili kujenga imani kwa wananchi na kuimarisha utendaji wa taasisi za umma.

"Mwalimu Julius Nyerere, Baba wa Taifa, aliwahi kusema kuwa "Uongozi ni dhamana, na kila kiongozi anapaswa kuwa mtumishi wa watu, si mtawala wa watu." Hili linatufundisha kuwa katika nafasi zetu mbalimbali za uongozi, tunapaswa kuweka mbele maslahi ya wananchi kwa kuzingatia maadili mema na kupinga rushwa kwa vitendo. Rushwa sio tu inaharibu mifumo ya kiutawala, bali pia inadidimiza maendeleo ya kijamii na kiuchumi, ikiwemo huduma kwa wananchi, elimu bora, na haki kwa wote".

Kwa upande wake Kamishna wa Maadili Mhe Jaji Mstaafu Sivangilwa Mwangesi ametumia nafasi hii kutoa wito kwa washiriki kuwa kila mmoja anapaswa kuwa balozi wa maadili na kuhamasisha utamaduni wa uwajibikaji na uadilifu ndani ya Taasisi aliyoko na kwingineko.

Kwani suala la Maadili na Uongozi bora ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano wa wadau wote ikiwemo Taasisi za Umma,Sekta binafsi na Asasi za Kiraia na hata Mashirika ya Kimataifa.

Awali Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo na ujuzi viongozi wa umma wa kina kuhusu maadili katika uongozi, utawala bora, matumizi ya fedha za umma, mifumo ya manunuzi, utoaji wa huduma kwa wananchi, na jinsi ya kutambua na kuondoa migogoro ya kimaslahi.

“Mafunzo hayo yatasaidia katika kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kukuza Uadilifu (NACSAP), ambao unalenga kupunguza mianya ya rushwa na kuimarisha utawala wa sheria katika sekta ya umma.”amesema Prof. Sedoyeka

Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu Wizara ya Fedha Simbani Liganga,amesema mafunzo hayo yatachangia kujenga utumishi katika sekta ya umma na binafsi kuongozwa na uadilifu, uwazi, na uwajibikaji.





Post a Comment

Previous Post Next Post