TANZANIA YAPOKEA FARU WEUPE 17 KUTOKA AFRIKA KUSINI


 Na Kassim Nyaki, Ngorongoro Kreta, Arusha.

Serikali kupitia wizara ya Maliasili na Utalii kwa mara ya kwanza imepokea Faru weupe 17 kutoka kampuni ya AndBeyond ya nchini Afrika Kusini kwa lengo la kuimarisha shughuli za uhifadhi, utafiti na elimu katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Akipokea faru hao katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika kreta ya Ngorongoro tarehe 4 machi, 2025 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amesema mradi wa kuwaleta faru weupe Tanzania unalenga kuimarisha shughuli za uhifadhi na kupanua wigo wa watafiti ambao kupitia faru hao watasaidia kutoa elimu kwa wananchi na hata wageni wenye lengo la kujifunza kuhusu maisha ya wanyama hao.

Waziri Chana amebainisha kuwa faru hao 17 kutoka Afrika kusini ni awamu ya kwanza ambapo awamu ya pili itahusisha faru wengine 19 na kufikisha jumla ya faru 36 ambao watawekwa katika maeneo mengine ya uhifadhi nchini.

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro Dkt. Elirehema Doriye ameeleza kuwa faru ni miongoni mwa spishi zilizo katika hatari ya kutoweka kutokana na vitendo vya ujangili na uharibifu wa makazi yao hivyo kuletwa kwa faru weupe kreta ya Ngorongoro ni hatua muhimu ya kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori na kuhakikisha vizazi vijavyo vina fursa ya kuwaona viumbe hao wa kipekee katika mazingira yao ya asili.

‘‘Ngorongoro tunajivunia kuwa moja ya maeneo machache barani Afrika ambapo faru weusi wanaendelea kustawi, Kwa kushirikiana na taasisi za utafiti za kitaifa na kimataifa, tumefanya tathmini ya kina kuhakikisha Ngorongoro inakidhi mahitaji ya faru weupe ili kuendelea kuimarisha uhifadhi”alisema Dkt.Doriye.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro -NCAA Jenerali Venance Mabeyo (Mstaafu) ameeleza kuwa, kuwasili kwa faru 17 katika kreta ya Ngorongoro ni kuandika historia mpya kwa Tanzania kwani itaongeza uhifadhi wa wanyama hao kwa kizazi kijacho.

Mabeyo ameeleza kuwa bodi ya wakurugenzi wa NCAA itaendelea kuisimamia menejimenti ili kuweka kipaumbele katika usalama wa faru na kushirikiana na wadau wa uhifadhi ili kuendeleza mikakati madhubuti ya kupambana na ujangili hasa kutumia mifumo ya kutumia teknolojia za kisasa, ikiwemo ufuatiliaji kwa drone, GPS tracking, pamoja na vikosi maalum vya doria kuendelea kufanya kazi usiku na mchana.

Kwa upande wake mwakilishi wa viongozi wa mila kutoka nchini Afrika Kusini, iNkosi Zwelinzima Gumede amebainisha kuwa lengo la kutoa Faru hao kwa Tanzania ni kuendeleza juhudi za Uhifadhi na kuongeza uzalishaji wa spishi ya Faru weupe katika nchi ya Tanzania pamoja na kuendelea kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Afrika kusini ambao uliasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Nelson Mandela.

“Kabla ya kuleta Faru hawa hapa Ngorongoro watalaam wetu walikuja kujiridhisha na Uhifadhi wa eneo hili na pia tumeona tafiti mbalimbali zinaonyesha hifadhi hii ni Nyumbani kwa faru tena wakiwa katika maeneo yao ya asili, hivyo hata faru hawa wapya tunaamini watakua vizuri na kuzaliana kwa wingi “amesema iNkosi Gumede.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, viongozi wa wilaya za Ngorongoro, Karatu na Monduli, Wadau wa uhifadhi kutoka kampuni ya AndBeyond nchini Afrika Kusini, bodi ya wakurugenzi wa NCAA na wadau wa sekta ya uhifadhi na utalii.   

Post a Comment

Previous Post Next Post