TFRA Yafanya Mazungumzo na Kampuni ya Median Global ya nchini Iran

Mwandishi Wetu,

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imekutana na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara kutoka Kampuni ya Median Global Company ya Iran kwa lengo la kujadili fursa za biashara na uwekezaji katika Tasnia ya mbolea nchini.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo tarehe 12 Machi, 2025 kwenye ofisi za Mamlaka Jijini Dar es Salaam.

Akiongoza mazungumzo hayo,  Kaimu Mkurugenzi Mtendaji  wa TFRA, Louis Kasera ameeleza uwepo wa fursa za biashara na uwekezaji kwenye tasnia ya mbolea ikiwemo kuingiza na kusambaza mbolea nchini, kujenga viwanda vya mbolea, kujenga viwanda vya kutengeneza vifungashio, kutoa huduma ya kufungasha mbolea, kushiriki katika shughuli za usafirishaji na usambazaji wa mbolea nchini.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Median Global Company, Saeed Nohehsara, alisema kuwa kampuni yao inajihusisha na biashara ya mbolea katika masoko mbalimbali duniani, hususan wakisafirisha mbolea kutoka Oman.

Ameeleza kuwa, kampuni hiyo na kampuni nyingine 8 nchini Iran wanajihusisha na uzalishaji wa mbolea aina ya Urea yenye ubora itakayoweza kuuzwa nchini Tanzania na kiasi kingine kusafirishwa nchi zilizoko ukanda wa Afrika.

Amesema, lengo kuu la kampuni hiyo ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha kusambaza mbolea wanayozalisha kwenye nchi nyingine barani Afrika.

Mazungumzo hayo  yanafungua milango ya biashara ya kampuni hiyo nchini ili kuimarisha upatikanaji wa mbolea bora   na kuleta tija  katika hivyo kukuza Sekta ya Kilimo nchini.



Post a Comment

Previous Post Next Post