Mwandishi Wetu,
Mfuko wa Pembejeo wa Kilimo wa Afrika (Africa Fertilizer Financing Mechanism – AFFM) umekutana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa mazungumzo ya kina kuhusu masuala muhimu yanayohusu sekta ya mbolea nchini, huku kipaumbele kikuu kikiwa ni afya ya udongo.
Katika kikao hicho, pande zote mbili zimejadili hali ya sasa ya matumizi ya mbolea, changamoto zinazojitokeza kwenye usambazaji na upatikanaji wake, pamoja na mikakati ya kuhakikisha wakulima wanapata elimu sahihi kuhusu matumizi bora ya pembejeo ili kuboresha tija.
Mkurugenzi Mkuu wa TFRA, Joel Laurent, amepongeza ushirikiano wa AFFM katika kuunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha udongo wa Tanzania unalindwa na kuboreshwa kupitia matumizi ya mbolea kwa kuzingatia mahitaji halisi ya udongo wa maeneo mbalimbali. “Afya ya udongo ni msingi wa kilimo endelevu. Tunahitaji ushirikiano wa kimataifa kama huu ili kuhakikisha wakulima wetu wanapata maarifa, teknolojia na pembejeo zenye ubora unaohitajika,” alisema
Kwa upande wake, Afisa Uwekezaji wa AFFM, Maria Theresa, amesema taasisi hiyo imejipanga kushirikiana na TFRA katika tafiti za udongo, kusaidia upatikanaji wa taarifa sahihi za kijiografia na kitafiti, na kuimarisha mifumo ya kifedha kwa ajili ya upatikanaji wa mbolea kwa wakulima wadogo.
Kikao hicho kimehitimishwa kwa makubaliano ya kuandaa mpango wa pamoja wa utekelezaji, utakaojumuisha kampeni za uhamasishaji kuhusu afya ya udongo, mafunzo ya kitaalamu kwa maafisa ugani na wakulima, pamoja na kuimarisha taratibu za udhibiti wa ubora wa mbolea nchini.