PROF KABUDI AKUMBUSHA MISINGI YA HABARI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

 




 WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Paramagamba Kabudi, ametaja mambo matano ya msingi ambayo sekta ya habari inapaswa kutekeleza kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.


Akifafanua, Profesa  Kabudi amesema jukumu la kwanza ni kuwajulisha wananchi kuhusu haki na wajibu wao, la pili kutoa elimu juu ya sera za wagombea, na la tatu kuibua pamoja na kufuatilia ukiukwaji wa sheria za uchaguzi.


Aidha, ametaja jukumu la nne kuwa ni kuhamasisha ushiriki wa makundi maalum, ikiwemo vijana na wanawake, huku la tano likiwa kupambana na taarifa potofu na kuepuka kuzisambaza.


Profesa Kabudi ameyasema hayo katika Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Habari na Utangazaji Kanda ya Mashariki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, uliofanyika jijini Dar es Salaam.


Aliongeza kuwa utekelezaji wa majukumu hayo unapaswa kuzingatia taaluma, weledi na maadili ya uandishi wa habari.

Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari Wakili Patrick Kipangula, amesema ni kosa la jinai kwa waandishi wa habari kufanya kazi hiyo bila kuwa na ithibati.


Kipangula alisema hayo wakati akiwasilisha mada katika mkutano wa wadau wa sekta ya habari na utangazaji kanda ta mashariki, kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.


"Ukisoma kifungu cha 19 cha Sheria ya Huduma za Habari inaeleza kuwa mtu yoyote anayetaka kufanya kazi za uandishi wa habari ni lazima awe amepewa ithibati na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, kwa hiyo hakuna mtu yoyote anaruhusiwa kufanya kazi yoyote ya kihabari isipokuwa tu awe amepewa ithibati na bodi, kwa hiyo waandishi ambao wanataka kufanya kazi ya kuripoti taarifa za uchaguzi wahakikishe wamepewa ithibati" alisema Kipangula.

Mwisho

Post a Comment

Previous Post Next Post