Na Mwandishi Wetu,
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda leo tarehe 12.03.2025 amewasilisha mafanikio ya TRA kwa kipindi cha miaka 4 ya Serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. Samia Suluhu Hassan na kueleza kuwa TRA imeongeza makusanyo ya Kodi kwa asilimia 78 tangu Rais alipoingia madarakani.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema kwa kipindi cha miezi nane mfululizo kuanzia Julai 2024 mpaka Februari 2025 TRA imekusanya kiasi cha Shilingi Trilioni 21.200 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2020/2021 ilikusanya Sh. Trilioni 11.9 sawa na ongezeko la asilimia 78 na ukuaji wa asilimia 17.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema makusanyo yaliyofanywa katika kipindi cha Serikali ya awamu ya 6 yamevunja rekodi ya makusanyo tangu kuanzishwa kwa TRA mwaka 1996 na hayo yote yametokana na maelekezo yanayotolewa na Mhe. Rais.
Amesema mafanikio mengine yaliyopatikana ni kuwezesha kukua kwa biashara na uwekezaji nchini wakishirikiana na Taasisi nyingine kama TIC katika kuvutia wawekezaji na kwa upande wa marejesho ya Kodi kwa Wafanyabiashara kwa kipindi cha miezi 8 wamelipa Sh. Trilioni 1.171 wakati kipindi kama hicho miaka minne iliyopita ililipwa Sh. Bilioni 92.
Kwa upande wa Mifumo amesema upo mfumo wa TANCIS ulioboreshwa unaofanya kazi za Forodha na mfumo wa IDRAS unaoshughulikia Kodi za ndani unaowezesha Mlipakodi kujihudumia mwenyewe hali iliyopunguza Watumishi wa TRA kukutana na Walipakodi.
Kamishna Mkuu Mwenda ameeleza kuendelea kuimarika kwa nidhamu miongoni mwa Watumishi huku akiainisha kuwepo kwa Watumishi 15 waliofukuzwa kazi kwa makosa mbalimbali ya kinidhamu, 6 wamepunguziwa mishahara, 12 wameshushwa vyeo na mishahara na Watumishi 22 wamepewa onyo la maandishi.
Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa idadi ya Watumishi wa TRA kutoka 4749 miaka minne iliyopita na kufikia Watumishi 6989 mwaka huu ambapo wanatarajia kuajiri Watumishi wapya 1596 watakaofanya Mamlaka iwe na Watumishi 8585 sawa na ongezeko la asilimia 80.
Kamishna Mkuu Mwenda ameeleza kuwa Elimu kwa Mlipakodi ni miongoni mwa vitu vilivyochangia kuongeza kwa makusanyo ya Kodi pamoja na Shukrani kwa Mlipakodi ambapo ameenda mikoa yote kuwashukuru Walipakodi na kusikiliza changamoto zao pamoja na kuzipatia ufumbuzi.
Amesema mwelekeo wa TRA ni kuendelea kutekeleza kwa vitendo maagizo wanayopatiwa na Mhe. Rais ili kuweka mazingira mazuri kwa Walipakodi na kuongeza makusanyo ya Kodi.



