WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAJIIMARISHA KIUTENDAJI.

 


Na Sixmund Begashe - Dodoma

Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kujiimarisha katika Ufuatiliaji na Tathmini ya  utendaji wa shughuli mbalimbali za Serikali zinazofanywa kupitia idara, vitengo na taasisi zake ili kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yake.

Akifungua kikao kazi cha wataalam wa Ufuatiliaji na Tathmini wakiwemo M&E Champions  kutoka idara, vitengo na taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii, Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Shughuli za Serikali, kutoka Ofisi ya  Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bi. Sakina Mwinyimkuu amewataka washiriki  kujiimarisha zaidi kielimu katika suala zima la  Ufuatiliaji na Tathmini (M&E) ili kupata uelewa mpana maana kazi yao ni muhimu katika kuchochea ufanisi na mafanikio makubwa kazini.

Bi. Mwinyimkuu ameipongeza Wizara hiyo kwa kuandaa mafunzo hayo yenye lengo la kutoka na nyaraka muhimu zitakazo imarisha zaidi  Upimaji na Ufuatiliaji wa utekelezaji wa kazi za Wizara.

"Ninyi ndio chachu ya Mabadiliko ya utendaji mzuri kwenye Taasisi zenu, hakikisheni mnafuatilia na kutathmini mipango kazi iliyopo, elimisheni watendaji ili watekeleze kazi zao kulingana na wakati uliopangwa na kwa tija iliyokusudiwa". Bi. Mwinyimkuu.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini Wizara ya Maliasili na Utalii Bi. Bure Nassibu, amesema Wizara hiyo imejipanga kikamilifu katika kuhakikisha wataalam wake wanapata mafunzo ya mara kwa mara ili kuwapatia uwezo wa Kufuatilia, Kutathmini na kuandaa Taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Taasisi na Idara zao. 

Mafunzo hayo yanayowezeshwa na wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, yatafanyika kwa siku 12 huku wataalam hao  wakitarajiwa kutoka na nyaraka muhimu za kuimarisha Ufuatiliaji na Tathmini katika Wizara

Post a Comment

Previous Post Next Post