
Na Mwandishi wetu- Berlin Ujerumani
Wizara ya Maliasili na utalii kupitia taasisi zake za Bodi ya Utalii Tanzania(TTB), Shirika la hifadhi za Taifa(TANAPA) na Mamlaka ya Uhifadhi wa Eneo la Ngorongoro(NCAA) imeendelea kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii nchini.
Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula(Mb) alipotembelea banda la Maonesho la Tanzania katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii yanayofanyika jijini Berlin Nchini Ujerumani(ITB BERLIN) ambapo Mhe. Kitandula yupo huko kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa umoja wa mataifa katika sekta ya utalii.
Aidha Mhe. Kitandula alipata wasaa wa kuongea na baadhi wa wadau wa utalii ambao walitembelea banda la Tanzania na wengi wao walimueleza kuwa wamefurahishwa na jinsi nchi ya Tanzania ilivyojipanga katika kukuza sekta ya utalii kwa kutangaza vivutio adimu na vya asili vinavyopatikana katika maeneo ya Tanzania Bara na Visiwani.
Mhe. Kitandula hakusita kuwakaribisha wadau hao kuja kuwekeza katika sekta ya utalii hasa katika upande wa malazi kwa kujenga hoteli katika maeneo ya hifadhi za wanyama na misitu. Mhe Kitandula alipotembelea maonesho hayo aliongozana na Balozi wa Tanzania Nchini Ujerumani, Mhe. Balozi Hassan Mwamweta.
Mkutano wa huo wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikiwa Utalii, unalenga kuwa na mjadala mpana wa namna bora ya kuongeza uwekezaji katika sekta ya utalii kwa kuwa utalii ni kitovu cha kujenga maridhiano na kutatua migogoro ili kuwa na Amani na Maendeleo endelevu katika sekta ya utalii.