TFRA YASHIRIKI MKUTANO WA 3 WA G25 WA WADAU WA KAHAWA

Mwandishi Wetu,DAR ES SALAAM, 

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imeshiriki Mkutano wa 3 wa G25 wa wadau wa kahawa za Afrika, uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, kuanzia tarehe 21 hadi 22 Februari 2025.

Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Bw. Joel Laurent, pamoja na timu ya wataalam wa biashara wa mamlaka hiyo, walihudhuria mkutano huo ambao uliwakutanisha viongozi wa serikali kutoka nchi 25 zinazozalisha kahawa.

 Mkutano huo ulibeba  kaulimbiu inayosomeka “Fungua Fursa za Ajira kwa Vijana Kutoka Kwenye Tasnia ya Kahawa.”

Mnamo tarehe 21 Februari, Mawaziri wa Kilimo wa nchi hizo walijadili na kuandaa rasimu ya Azimio la Kahawa la Dar es Salaam, ambalo linatarajiwa kusainiwa na mataifa yote 25 yanayozalisha kahawa kwa ajili ya utekelezaji wake. 

Aidha, vijana wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) Tanzania walitoa mada kuhusu ushiriki wao katika mnyororo wa thamani wa kahawa, huku wakitambua mchango wa taasisi mbalimbali, ikiwemo TFRA, inayotoa mafunzo ya matumizi sahihi ya mbolea kwa vijana wanaoshiriki katika mradi wa BBT.

Akifunga mkutano huo tarehe 22 Februari 2025, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, alieleza dhamira ya Serikali yake ya kuongeza uzalishaji, ubora, na tija ya zao la kahawa. 

Rais Dkt. Samia alisisitiza kuwa, serikali itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima wa kahawa ili kufanikisha dhamira hiyo.

Mkutano huu wa G25 umelenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya kahawa na kuboresha mchango wa vijana katika kilimo kupitia uwezeshaji katika kilimo cha kahawa.



Post a Comment

Previous Post Next Post