Mwandishi Wetu,
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) inaendelea kuwezesha ukuaji wa viwanda vya mbolea nchini kwa kuwajengea uwezo wazalishaji wa kati na wadogo wa pembejeo hiyo.
Katika kikao muhimu kilichofanyika tarehe 5 Februari 2025, TFRA ilikutana na wazalishaji wa mbolea kutoka viwanda 14 kujadili utekelezaji wa takwa la sheria ya Mazingira kuhusu tathmini ya mazingira, pamoja na changamoto na fursa zinazokabili sekta hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Bw. Joel Laurent, aliwahakikishia wazalishaji kuwa Mamlaka hiyo si chombo cha udhibiti pekee bali ni mshirika wa maendeleo katika kukuza uzalishaji wa mbolea ndani ya nchi. Alisisitiza kuwa:
Katika kutatua changamoto ya mitaji TFRA imewaeleza wazalishaji hao uwepo wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), iliyoonesha utayari wa kutoa mikopo kwa wazalishaji wadogo na kwa riba nafuu
Kuhusu suala la uzingatiaji wa viwango na uhifadhi wa mazingira Laurent amesema Ili kuhakikisha viwanda vinakidhi matakwa ya kisheria na kimazingira, TFRA inashirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ili kutoa elimu na mwongozo wa utekelezaji wa sheria bila kuwa kikwazo kwa maendeleo ya viwanda.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja, Louis Kasera amewashauri wazalishaji wa mbolea kuunda chama chao rasmi kwa ajili ya kuwa na sauti ya pamoja kwenye mijadala kuhusu uwekezaji wao kwenye uzalishaji wa mbolea.
Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, TFRA inalenga kuhakikisha wakulima wanapata mbolea bora kwa gharama nafuu, huku ikijenga mazingira wezeshi kwa wazalishaji wa ndani.