Na Lusungu Helela- ARUSHA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema zaidi ya asilimia 40 ya Watumishi wa Umma hawafanyi kazi licha ya kulipwa mshahara kila mwezi.
Amesema hiyo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa hivi karibuni na Tume ya Utumishi wa Umma nchini
Mhe. Simbachawene amesema hayo leo jijini Arusha wakati akifunga Kikao kazi cha tano cha Serikali Mtandao ambapo amesema Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma wanawajibu wa kuhakikisha kila mtumishi anatekeleza majukumu yake ipasavyo.
‘’Watumishi ni lazima wafanye kazi kwani wasipofanya kazi wanakuangusha wewe Mkuu wa Taasisi, lazima tuwe na jamii inayoandaliwa kufanya kazi’’ amesisitiza Mhe. Simbachawene
Amefafanua kuwa kwa mujibu wa tafiti hiyo, wavivu, wazembe, wagonjwa pamoja na waliosusiwa kutokana na vipaji na uwezo wao ni asilimia 40 ya Watumishi wanaolipwa pasipo kufanya kazi
Amewataka Wakuu hao kuwatumia Watumishi wa Umma wenye vipaji na uwezo badala ya kuwafanyia fitina na hujuma hali inayopelekea kurudisha nyuma maendeleo ya nchi
Amesema hali hiyo imesababisha kutokuwepo kwa urithishanaji wa madaraka jambo ambalo limechangia kudhoofika kwa Taasisi pale kiongozi wa Taasisi anapostaafu au kuhama
Aidha, Mhe. Simbachawene amesema kumeibuka tabia ya baadhi ya Watendaji wakuu hao pindi Mtumishi mwenye sifa za ziada anapohamia kwenye Taasisi anayoiongoza hupata hofu na kutompangia najukumu kwa hisia kuwa ametumwa kumchunguza a au kuchukua nafasi yake
Ameeleza kuwa tabia hiyo kwenye utumishi wa umma haikubaliki na wale wenye tabia hiyo wajirekebishe haraka kwani Taasisi hizo wanazoziongoza ni za umma na sio mali yao binafsi
Katika hatua nyingine, Kutokana na ongezeko la matumizi ya simu kwa wananchi, Mhe. Simbachawene amezitaka Taasisi za Umma kutoa huduma za kidijitali kutokana na fursa hiyo
Vilevile, Mhe. Simbachawene amezitaka Taasisi za Umma ambazo hazijaanza kutumia mfumo wa kidijitari wa e-Mrejesho ziingie mara moja la sivyo zitachukuliwa hatua kali na Ofisi anayoiongoza.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, ( e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba aliwashukuru washiriki wa kikao hicho cha jumla 1526 ya ushiriki wao ambapo jumla ya mada 18 ziliwasilishwa ikiwa ni pamoja na kujiwekea mikakati ya kukabiliana na changamoto za usalama wa mtandao Serikalini.
Amesema kikao hicho kimejadili changamoto mbalimbali zinazoikabili Serikali Mtandao pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kuchangamkia fursa ya kujifunza teknolojia mpya zinazoibukia ili kuendana na mabadiliko yanayotokea duniani kote.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mhe.Festo Kiswaga ameishukuru e-GA kwa kuendelea kuuamini Mkoa wa Arusha ikiwa ni mara ya tano sasa vikao hivyo vimekuwa vikifanyika Mkoani humo hali iliyopelekea Mkoa huo kuwa wanufaika wakubwa wa kiuchumi pamoja na kuwa wadau namba moja wa matumizi ya Serikali Mtandao.
Naye Katibu Mkuu-IKULU, Bw. Mululi Mahendeka amesema Ofisi yake itasimamia na kufanyia kazi maazimio yote yaliyowasilishwa leo na kuhakikisha utekelezaji wake unawasilishwa katika kikao kijacho
Pia, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya e-GA, Dkt. Jasmine Bunga amesema kikao kazi hicho kimekuwa muhimu kwa washiriki ambapo mbali ya kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili pia wamejiwekea mikakati ya kuendelea kujenga Serikali ya kidigitali
Amesema lengo ya kujiwekea mikakati hiyo ni kuhakikisha Serikali inapiga hatua kubwa kwenye matumizi ya mifumo ya TEHAMA itakayoleta tija na ufanisi wa hali ya juu katika utoaji wa huduma bora za haraka na za uhakika kwa wananchi.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiRliw70eYbUTk_ogYy3M7_Dj7NhGRe3B0LrmUo1ZlhY4qmizGrPv6_Dl4HMK3S1e_51Qr9RH_NKD-KjXInrxE3bqGbTgBg1z20X2pAdjG2RaR0R0oL56cxk-hHtsrYdbIpRSNUR2Ba8uS-CMtJm9oKdbMhiWI24oFGXlNK9qhRL6HgDFyUK1Ga3A/s16000/1.jpeg)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEj4hKNiGjVRZCFXXj5Xv3r-dUaoafc56q-P1A9n7BwOms5f-q4Qdau7H79GeGQYoS9_imfLEl98MpzYD55fEuI5v7lei8YoxHxxBQwSaP_j7ZrWELKeZoA6gtApCJnzcgg5YInexmWQ8uXiowEHFmcJARdTSGoFhNForkdrGFbdRTWOB3N0nUeA8A/s16000/2.jpeg)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEj5CMGI7ES69PsAU_FLXEjGZT2eulnkG9Ku8DD8b94mbyz-D5Vt-Q2qzPHX1NAlaUD_benowmyvqlMmKs5mVRyTXoml5VWJGfATcxoT5lZASY1E_zKQ5Ke29jpOPzYgAN83pTd315Q3OwMBxRfa-wI9ooQfrpHGSazY-ZkoYToF4SCNhsxBF_s_Fw/s16000/4.jpeg)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgfHiv9eMlRewDvskbByzUZKMlJfE5RizAvPpcy9O2D7BUfHoZh3mlVEOC3F3SAxQ4C9tjuffSuLtFDzSJn8n5Gf5GlIqXLIH0indRsNtpy5EVhsOiKewe-az6jx0nydNtAKLPu0OAIAskoPIAbUk1BzyPMFtYjaDhagZ3j7bzi4MmTeox5UXA5nQ/s16000/5.jpg)