
VIONGOZI na wadau mbali mbali wa NGO's wamepata elimu ya kodi hususani kuhusu sheria za kodi zinazohusu uendeshaji mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs).
Semina hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelelekezo ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) CPA Yusuph Juma Mwenda aliyoyatoa wakati wa kikao chake na wafanyabiashara wa mkoa wa Singida hivi karibuni.
Semina hii imehusisha Elimu ya kodi ya namna ya kuwasilisha ritani za kodi katika mfumo wa TRA pamoja na uzingatiaji wa sheria za kodi zinazohusu uendeshaji wa NGOs.
Akifungua semina hiyo, Msajili Msaidizi wa NGOs mkoani Singida Bw. Patrick Kasango ameishuishuru TRA kwa kuwa na utaratibu mzuri wa kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya walipakodi ikiwemo la mashirika yasiyo ya kiserikali na hivyo amewahimiza viongozi wa NGOs kuzingatia elimu ya kodi watakayoipata na kulipakodi bila shurti “Semina hii ni muhimu sana, na niwaombe muizingatie ili muweze kulipakodi kwa hiari na kwa wakati” amesema Bw. Kasango kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa Singida.
Naye CPA Paul Walalaze Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania amesema TRA itaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali yakiwemo ya wafanyabiashara na watoa huduma ambao wanawajibika kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.
“Ni jukumu letu kutoa elimu ya kodi kwa walipakodi na watanzania kwa ujumla ili kuongeza ulipaji kodi kwa hiari na kwa wakati” amesema CPA Walalaze.
Kwa upande wake Mwakilishi wa NGOs mkoani Singida Bi. Happy Francis amemshukuru Kamishna Mkuu kwa kutekeleza ahadi yake ya kuwapa Elimu ya kodi viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali kwani hilo lilikuwa hitaji lao kubwa na litawasaidia kutimiza wajibu wao wa kulipakodi kwa hiari na kwa wakati.
“Tunamshukuru sana Kamishna Mkuu wa TRA CPA Yusuph Juma Mwenda kwa kutimiza ahadi yake nasi tunaahidi kutimiza jukumu letu la kulipakodi kwa maendeleo ya nchi yetu”, amesema Bi. Happy Francis.
Semina hiyo imetolewa na timu maalumu kutoka Dar-es-salaam ikiongozwa na Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi CPA Paul Walalaze na Meneja Msaidizi-Ukaguzi TRA Mkoa wa Singida CPA Iddy Omar, Afisa Mkuu Msimamizi wa Kodi Bw Hamad Mtery na Bi. Ernesta Shirima Afisa TEHAMA Mwandamizi.

Picha ya pamoja.