Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari amewataka washiriki wa kozi ndefu ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kundi la 13, kuendelea kuzingatia Sheria za bahari na usimamizi wa rasilimali zilizoko baharini.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameyasema hayo leo tarehe 25 Feburari, 2025 wakati akiwasilisha mada kwa washiriki hao kuhusu Sheria za Bahari na Antaktika pamoja na utunzaji wa maliasili za bahari kwenye mhadhara uliofanyika katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kilichoko Kunduchi, Jijini Dar es Salaam.
Akitoa mada katika mhadhara huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa mada hizo zimelenga kuwajengea uwezo washiriki wa kozi ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi juu ya masuala mbalimbali yanayohusu Sheria za bahari na rasilimali zilizoko baharini pamoja na Mikataba inayosimamia bahari kuu.
“Lengo kubwa ilikuwa ni kawajengea uwezo katika maeneo ya Sheria za Bahari na namna ambavyo sisi kama nchi tunashiriki katika kuzitekeleza sheria hizo.”
Aidha, Mhe. Johari amesema kuwa washiriki wa kozi hiyo wameweza kufahamu namna nchi inavyoshirikiana na nchi nyingine katika matumizi ya maeneo ya bahari hususani bahari kuu, pia washiriki hao wameelezwa juu ya ulindaji wa maliasili zilizoko baharini.
“Ni Mhadhara ambao ulikuwa umejikita katika Sheria za Bahari pia kuweza kuwafahamisha kuhusu matumizi sahihi ya bahari kuu na jinsi ambavyo nchi yetu inashirikiana na nchi nyingine.”
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Meja Jeneral Wilbart Augustin Ibuge akimkaribisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali alieleza kwa kifupi kuwa Kozi hiyo inashirikisha Washiriki 61 kutoka mataifa 16 duniani ambapo Tanzania ndio mwenyeji, kozi hiyo ni ya 13 toka kuanzishwa kwake na ilianza toka Septemba 2024 inatarajia kukamilika mnamo Julai 2025.
“Kozi hii inashirikisha Maafisa kutoka mataifa takribani 16 kutoa maeneo mbalimbali duniani, naamini ujio wako utawasaidia sana washiriki kuweza kufahamu masuala ya kisheria
uliyowaandalia.”