KAMISHNA IDARA YA UPELELEZI AFANYA ZIARA YA KUKAGUA SHUGHULI ZA UDHIBITI MAGENDO KATIKA UKANDA WA PWANI YA BAGAMOYO

 







KAMISHNA wa Idara ya Upelelezi wa Kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Hashimu Ngoda amefanya ziara ya kutembelea vituo vya forodha ukanda wa pwani katika maeneo ya Kunduchi, Mbweni pamoja na Bagamoyo lengo likiwa ni kuangalia utendaji wa shughuli za forodha katika kudhibiti shughuli za magendo.

Hayo yamebainishwa leo na Kamishna Ngoda katika kituo cha Bagamoyo Mkoani Pwani ambapo amewataka wafanyakazi kuzingatia taratibu za kimaadili ili kuepuka upotevu wa mapato katika vituo vya forodha pamoja na kuwasihi wafanyabiashara kutumia njia rasmi ili kuepuka usumbufu wa kukamatwa na vyombo vya dola.

Aidha, Kamishna Hashim Ngoda amesema kuwa kituo cha Bagamoyo ni moja ya kituo cha kimkakati kwani kimekuwa kikiunganisha na kuhudumia Zanzibar na Bara katika mikoa ya Dar es salaam na Pwani huku kikiwa ni kichocheo cha shughuli za kiuchumi kwa wakazi wa Bagamoyo.

Pia, Kamishna Ndoda amewasihi wafanyabiasara kukitumia kituo cha Bagamoyo kwani ni kituo chenye eneo la kutosha na usalama imara sambamba na watumishi wachapakazi kwaajili ya kuwahudumia wafanyabiashara muda wote wa kazi katika kuchakata upitishaji wa biashara zao.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya pwani Mh. Shaibu Ndemanga ametoa wito kwa wakazi wa Bagamoyo kulipa kodi kwa hiari Pamoja na kudai risiti mara tu wafanyapo manunuzi huku akivitaka vyombo vya dola wilayani hapo kutumia boti iliyonunuliwa katika kudhibiti magendo katika ukanda huwo wa pwani huku akisisitiza kuwa lengo la boti hiyo ni kufanya doria mbalimbali za mapato.

Kwa upande wake Afisa Mkuu Bandari ya Bagamoyo, Mussa Kondo amesema kuwa hatua wanazochukua katika kudhibiti magendo ni kufanya doria mara kwa mara hadi kupelekea kupungua kwa magendo kituoni hapo Pamoja na kuongezeka kwa uelewa kwa wafanyabiashara kuhusu athari za magendo.

Pamoja na hilo Afisa Kondo amewasishi wafanyabiashara kuachana na njia za magendo huku akiwataka kutumia njia zilizo rasmi katika kupitisha biashara zao kwani kufanya hivyo kutasaidia kulinda mitaji yao kwa kuepuka kukamatwa kwa kutokuwa na nyaraka za kutosha.

Ziara ya Kamishna itachangia kupunguza shughuli za magendo kwa wafanyabiashara kwa ukanda wa pwani na kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato pamoja na uboreshaji wa huduma kwa kukumbusha taratibu za kimaadili kwa watumishi ili kuepuka upotevu wa mapato katika vituo vya forodha katika ukanda huwo.

Post a Comment

Previous Post Next Post