Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja amewataka watumishi wa Ofisi hiyo kuendeleza ushirikiano na kuimarisha ushawishi kwa wadau wa kitaifa na kimataifa katika kusukuma agenda ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini.
Mhandisi Luhemeja amesema hayo Desemba 17, 2024 wakati wa mkutano wake na watumishi wa ofisi hiyo uliolenga kutathimini mafanikio yaliyopatikana mwaka 2024 na kujadili mikakati ya vipaumbele kwa mwaka 2025.
Amesema katika mwaka 2024 watumishi wa Ofisi hiyo wamefanya kazi kubwa na kupata mafanikio makubwa katika kusimamia sekta za hifadhi ya mazingira nchini na hivyo kuendelea kujenga imani kwa viongozi wakuu wa Serikali pamoja na wadau wa kitaifa na kimataifa.
“Tarehe 9 hadi 10 Septemba, 2024 tulifanya mkutano wa wadau wa mazingira, uliohusisha Viongozi Wakuu wa Serikali, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri, hii imedhirisha imani ya Serikali na wadau kwa ofisi hii katika suala la usimamizi wa sekta ya hifadhi ya mazingira, nawasihi tuwe mabalozi," amesema Luhemeja.
Aidha Luhemeja amesema agenda ya uhifadhi wa mazingira ni suala mtambuka linalohitaji ushirikiano na wadau mbalimbali na kwa kutambua umuhimu huo Ofisi ya Makamu wa Rais, imewateua Maafisa Viungo 26 wataokaofanya kazi na Maafisa Mazingira waliopo katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Ameongeza kuwa jukumu la Maafisa Viungo wa Ofisi ya Makamu wa Rais, ni kuainisha mafanikio na changamoto mbalimbali za uhifadhi na usimamizi wa mazingira zinazojitokeza katika Mikoa na Halmashauri za Wilaya na kutoa taarifa kwa Mamlaka za juu kwa ajili ya hatua za utekelezaji pale inapohitajika.
“Agenda ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira imeingizwa katika kipaumbele cha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na tutaanza kuitekeleza kuanzia Julai 2025, hivyo hatuna budi kujipanga ili tuweze kufanikisha utekelezaji wake kwa kuwawezesha Maafisa Viungo,” amesema Luhemeja.
Ameeleza kuwa katika mwaka 2025 Ofisi hiyo imepanga kusimamia kwa ukamilifu agenda ya nishati safi ya kupikia, usimamizi wa biashara ya kaboni na dhana ya kampeni ya upandaji miti ili ikiwa ni juhudi za kuimarisha sekta ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini.
Awali akiwasilisha Mada kuhusu Baishara ya Kaboni, Mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) Prof. Eliakim Zahabu amesema hadi sasa Kituo hicho kimeweza kusajili miradi 63 ya biashara ya kaboni kutoka kampuni mbalimbali.
Amesema kampuni nyingi zimeonesha kuvutiwa na sera za miongozo na kanuni zilizopo zinazosimamia biashara hiyo na hivyo kuongeza Imani ya Serikali kutoka kwa wadau wa mashirika ya kitaifa na kimataifa.
Kikao hicho cha siku kilihudhuriwa na Viongozi na Watendaji waandamizi wa Ofisi hiyo akiwemo Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Bw. Abdallah Hassan Mitawi na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Bi. Christina Mndeme.