Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora na Utumishi wa Umma, George Simbachawene, akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wakurugenzi ya Uongozi Institute Balozi Ombeni Sefue Mara baada ya uzinduzi rasmi uliofanyika Hoteli ya Hyyat Regence jijini Dar es Salaam Leo Novemba 28, 2024.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora na Utumishi wa Umma, George Simbachawene, akiongozana na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhandisi Zena Said na Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wakurugenzi ya Uongozi Institute Balozi Ombeni Sefue kushoto Mara baada ya uzinduzi rasmi wa Bodi hiyo uliofanyika Hoteli ya Hyyat Regence jijini Dar es Salaam Leo Novemba 28, 2024.
………………..
SERIKALI imeiagiza Bodi Mpya ya Chuo Cha Uongozi kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali fedha ili kuifanya iwe Taasisi endelevu yenye nguvu na uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora na Utumishi wa Umma, George Simbachawene, , aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa akizindua bodi mpya ya wakurugenzi ya taasisi hiyo.
Alisema kuwa mchakato wa kujenga viongozi wa kiwango cha juu lazima uendelee bila kukatishwa tamaa.
Alisisitiza pia umuhimu wa kuwasilisha kwa ufanisi matokeo na athari za maendeleo ili kuhakikisha ukuaji endelevu wa taasisi hiyo hapa Tanzania na kote Afrika.
Bodi mpya ya wakurugenzi inayoongozwa na Balozi Ombeni Sefue, ina wajumbe wakiwemo Balozi Theresa Zitting (Balozi wa Finland nchini Tanzania), Dkt. Laura Torvinen, Balozi wa zamani wa Finland nchini Tanzania na Dkt. Brian Cawley, Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Taasisi ya Utawala wa Umma.
Wengine ni Balozi, Meja Jenerali (mstaafu) Gaudence Millanzi, Begun Taj, Balozi wa zamani wa Tanzania, Prof. Samwel Wangwe, mstaafu Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Dkt. Hamis Mwinyimvua, Mhadhiri Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Simbachawene alisema kuwa Taasisi ya Uongozi imejijengea umaarufu kama taasisi ya kikanda inayolenga kuimarisha uwezo wa viongozi wa Afrika katika kusimamia maendeleo endelevu.
Aliongeza kuwa taasisi kama hiyo inahitaji wajumbe wa bodi yenye umaarufu wa kimataifa na uelewa mpana na kuongeza kuwa uteuzi wao unapaswa kutegemea sifa binafsi na uzoefu unaohitajika kusaidia malengo ya taasisi.
“Wajumbe wapya wa bodi wanakidhi vigezo vyote,” alisema Simbachawene. “Rais Samia Suluhu Hassan amewaamini katika nyadhifa hizi ili kuendeleza ukuaji wa bara hili. Tafadhali pokeeni uteuzi huu kwa heshima.”
Mwenyekiti mpya wa bodi, Balozi Ombeni Sefue, alithibitisha uwezo wa taasisi hiyo katika kukuza viongozi kote Afrika ili kushughulikia masuala muhimu yanayoathiri maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya bara hili.
Alisema kuwa mkazo wa Taasisi hiyo katika maendeleo ya kiuchumi na maamuzi umechangia miradi muhimu kama vile ujenzi wa Reli ya Kisasa ya mwendokasi (SGR) na kukuza myororo wa thamani wa uongozi
Balozi Sefue aliongeza kusema kuwa Taasisi hiyo imeendelea kuimarisha uwezo wa mawaziri, viongozi wa sekta binafsi,wakuu wa mikoa na wilaya.
“Tunaendelea kuhakikisha kuwa Taasisi inatimiza lengo lake la kuimarisha viongozi katika ngazi za kitaifa na kikanda ,” alisema.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo, alielezea mafanikio kadhaa ikiwemo kuanzishwa kwa programu ya uongozi wa wanawake.
Alithibitisha kuwa taasisi hiyo iko katika hali nzuri kifedha na inapata mchango mkubwa kutoka kwa vyanzo mbalimbali vinavyosaidia juhudi zake.
Singo alisema kuwa uongozi na wafanyakazi wa Taasisi ya Uongozi wameonesha kujitolea bila kuchoka, jambo ambalo limechangia mafanikio na athari zinazozidi kuongezeka za taasisi hiyo.