Na mwandishi wa Dar es salaam,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, ameziagiza taasisi za umma kuhakikisha zinatekeleza sheria ya usalama na afya mahali pa kazi ili kulinda nguvu kazi ya Taifa na kuongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi.
Akizungumza katika ziara yake aliyoifanya katika Ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) mnamo Novemba 16, 2024, katika kuhitimisha zoezi la ukaguzi wa mifumo ya Utumishi wa Umma uliofanyika kwa taasisi za serikali zipatazo 160 Mhe. Simbachawene amesema moja ya vipengele kati ya vipengele 13 ambavyo tume ya Utumishi wa Umma iliyokuwa inakagua ni Pamoja na na utekelezaji wa sheria na kanuni zinazohusiana na usalama na afya mahali pa kazi.
“Sote tunafahamu kuwa kinga ni bora kuliko tiba. Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi Na. 5 ya Mwaka 2003 inaelekeza maeneo yote ya kazi nchini kuwa na Mifumo madhubuti ya kuwakinga Wafanyakazi dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.
Aidha, kwa kutambua umuhimu wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Wizara yangu ilitunga Kanuni ya 105 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022 inayoelekeza Waajiri kuchukua tahadhari zote dhidi ya ajali na magonjwa mahali pa kazi.
Nichukue fursa hii kuwapongeza sana OSHA kwa kuendelea kuisimamia Sheria hii na kuhakikisha kuwa Waajiri wanasimamia kikamilifu masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi ili kuwakinga watumishi wa Umma dhidi ya magonjwa, ajali na hata vifo.“ alisema
Waziri Simbachawene alitumia fursa hiyo pia kutoa pongezi kwa OSHA kwa kuendelea kusimamia vyema utekelezaji wa sheria hizi na kuhakikisha waajiri wanachukua hatua za kujikinga na kuwalinda wafanyakazi wao.
“Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha wafanyakazi wa umma wanalindwa na kuwa na mazingira salama ya kazi. Tunapojali usalama wa wafanyakazi wetu, tunajenga Taifa lenye nguvu kazi imara,” aliongeza.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mhe. Jaji Mstaafu Hamisa Kalombola, alielezea kuwa ziara hiyo ni sehemu ya majukumu ya tume ya kufanya ukaguzi wa utekelezaji wa sheria mbalimbali za utumishi wa umma
Alisema kuwa Tume imejiwekea utaratibu wa kufanya ukaguzi katika taasisi mbalimbali na kwamba ziara hiyo inatoa fursa ya kuzungumza na wafanyakazi kuhusu masuala ya nidhamu na usalama.
“siku ya leo nimefarijika kushiriki nanyi OSHA katika kikao hiki baada ya kumaliza ukaguzi vilevile niwajuze kuwa tume hii katika kutekeleza jukumu lake la ukaguzi imejiwekea utaratibu ambapo viongozi wanapata nafasi ya kutembelea taasisi ambayo inakaguliwa kama ilivyofanyika leo
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA Bi. Khadija Mwenda alisema taasisi hiyo itaendelea kusimamia maagizo yote yaliyotolewa, kwa kuendelea kusimamia na kufanya kaguzi na kutoa elimu ya usalama na Afya na Afya Mahali Pa kazi.
“utekelezaji huu ndani ya serikali ni ishara kuwa Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anathamni wafanyakazi wa Tanzania kwa kutambua kuwa Taifa linahitaji nguvu kazi yenye afya ili kuleta maendeleo tarajiwa.
Lengo la OSHA ni kuhakikisha tunajenga nguvu kazi yenye afya na usalama kwa kuhakikisha kuwa maeneo ya kazi yanasimika mifumo ya kulinda wafanyakazi, ambapo kwa sasa tuna imani serikali ikiwa kama mwajiri na mtunga sera mbalimbali ni matarajio yetu kuwa waajiri wote watazingatia hili ili tulinde nguvu kazi ya taifa” alisema Bi. Khadija Mwenda.
Naye Bwana Mathew Kirama Katibu, Tume ya Utumishi wa Umma Umma amesema jukumu la Tume ya Utumishi wa Umma ni Kuhakikisha kuwa sera,sheria,Kanuni,Taratibu na miongozo hiyo inayotolewa na Ofisi ya Rais,Menejmenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inazingatiwa ipasavyo, na Tume hutekeleza jukumu hilo kupitia ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria katika usimamizi wa utumishi wa Umma. Ambapo katika ukaguzi huo jumla ya taasisi za Umma zipatazo 160 zimekaguliwa kwenye vipengele 13 kuhusiana na uzingatiaji wa sheria.
Waziri wa Nchi Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, akitoa hotuba katika zoezi la kuhitimisha ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria katika usimamizi wa utumishi wa umma leo tarehe 16 Novemba 2024 uliofanyika katika ofisi za OSHA Kinondoni, jijini Dar es Salaam, ambapo zoezi hilo limehudhuliwa na Menejimenti ya Utumishi Pamoja na Wakala wa Usalama na Afya mahali pa kazi.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew kirama akitoa hotuba mbele ya Waziri wa Nchi Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Wakala wa Usalma na Afya mahali pa Kazi (OSHA) katika zoezi la kuhitimisha ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria katika usimamizi wa utumishi wa umma leo tarehe 16 Novemba 2024 uliofanyika katika ofisi za OSHA Kinondoni, jijini Dar es Salaam.