NAIBU WAZIRI WA MAJI AMTAKA MKANDARASI ANAYEJENGA MRADI WA MAJI MANGAKA KUFANYA KAZI MASAA 24

 

Naibu Waziri wa maji Mhandisi Kundo Mathewe katikati,akitoa maelekezo kwa kwa wasimamizi wa mradi wa maji Mang’aka na mkandarasi wa mradi huo baada ya kukagua ujennzi wake,kushoto Mkurugenzi wa usambazaji wa mamlaka ya maji Masasi Nachingwea(Manawasa)Mhandisi Janeth Mawenya na kulia Mkuu wa wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara Christopher Magala.

Naibu Waziri wa maji Mhandisi Kundo Mathewe wa pili kushoto,akimsikiliza mkurugenzi wa usambazaji wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Masasi-Nachingwea(MANAWASA)Mhandisi Janeth Mawenya kushoto,baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji wa miji 28 wa Mangaka unaotelekezwa na Mkandarasi kampuni ya Afcon kwa gharama ya zaidi ya Sh.bilioni 38,kulia Mkuu wa wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara Christopher Magala.

………..

Na Mwandishi Wetu, Nanyumbu

NAIBU Waziri wa maji Mhandisi Kund Mathew,amemtaka mkandarasi Kampuni ya Afcons inayojenga mradi wa maji wa miji 28 wa Mangaka wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara, kufanya kazi usiku na mchana ili iweze kukamilisha mradi huo kwa wakati.

Mradi wa maji Mangaka ambao chanzo chake ni mto Ruvuma,unajengwa na Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya India kupitia Mkandarasi kampuni ya M/S AFCONS ambao utahudumia wakazi wa mji wa Mangaka wilaya ya Nanyumbu wanakabiliwa na changamoto kubwa na ya muda mrefu ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.

Naibu Waziri Kundo Mathew,ametoa agizo hilo jana baada ya kutembelea mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya Afcons ya India kwa gharama ya Dola milioni 16 sawa na Sh.bilioni 38 za Kitanzania na ujenzi wake umefikia asilimia 56.

Alisema,mradi huo ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo Serikali imeshatoa kiasi cha Sh.bilioni 20 kati ya Sh.bilioni 38 kwa mkandarasi.

Waziri Kundo alitaja kazi zinazotekelezwa katika mradi huo ni ulazaji bomba kutoka kwenye chanzo hadi kwenye tenki la lita milioni 5.5,kulaza bomba kutoka kwenye tenki la awali hadi tenki la kutibu maji umbali wa kilometa 2.5 na kujenga mtandao wa maji kwenda wananchi umbali wa kilometa 68.

Alisema,hakuna changamoto yoyote itakayomfanya mkandarasi kushindwa kukamilisha kazi hiyo kwa muda uliopangwa,kwani Serikali imetoa Sh.bilioni 20 na anatakiwa kukamilika mradi huo mwezi Disemba mwaka huu.

Amemtaka kuongeza nguvu kazi ya watu,kwani waliopo ni wachache ambao hawatawezi kukamilisha kwa ujenzi kwa wakati na Serikali haitaongeza muda wa ziada.

“Matarajio ya Mheshimiwa Rais mradi huu ukamilike haraka iwezekanavyo kama yalivyo makubaliano kwenye mkataba ili mradi huu ulete matarajio yaliyokusudiwa ya kumaliza adha ya maji safi na salama kwa wananchi wa Mji wa Mangaka”alisisitiza Kundo.

“tunataka mradi huu uanze kutoa maji safi na salama haraka iwezekanavyo ili kuokoa wananchi na magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyokuwa safi na salama”alisema Kundo.

Alisema,maji ni uhai na maji ni uchumi hivyo kupitia falsafa ya Rais Samia ya kumtua mama ndoo kichwani katika umbali usiozidi mita 400 na mradi huo utachochea kukua kwa uchumi wa wakazi wa Nanyumbu na kuharakisha maendeleo ya mkoa wa Mtwara kwa ujumla.

Amewaomba wananchi wa Mkoa wa Mtwara,kuhakikisha wanautunza chanzo cha maji cha mto Ruvuma kwa kutofanya shughuli za kibinadamu zinazoweza kusababisha mto huo kukosa maji na mradi kutoleta tija iliyokusudiwa na Serikali.

“Nawaomba sana kupitia Serikali za mitaa,vijiji na wilaya na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Masasi na Nachingwea (MANAWASA), kuhakikisha chanzo hiki kinalindwa na kutoa elimu ambayo itawasaidia wananchi wetu kuachana na uharibifu wa mazingira hasa kwenye vyanzo vyetu vya maji”alisema Kundo.

Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Masasi- Nachingwea(MANAWASA) Kiula Kingu alisema,mradi huo utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 5.5 za maji kwa ajili ya wananchi wa wilaya ya Nanyumbu hasa wanaoishi katika mji wa Mangaka.

Alisema,hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 56 ya ujenzi wake ambapo tayari mkandarasi ameanza kazi ya ujenzi wa chanzo katika mto Ruvuma,kulaza mabomba urefu wa kilometa 56.9 kati ya kilometa 68.9.

Mkuu wa wilaya ya Nanyumbu Christopher Magala,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo kwani ni mradi wenye maana na faida kubwa sana kutokana na hali ya upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo kuwa kubwa ikilinganisha na maeneo mengine hapa nchini.

Magala,amempongeza Naibu Waziri Kundo,kwenda Nanyumbu kwani ziara yake itasaidia kusukuma ujenzi wa mradi huo na miradi mingine ya maji inayotekelezwa katika vijiji mbalimbali ili kuwaondolea wananchi wa Nanyumbu kero kubwa ya maji.

Alisema,kwa sasa upatikanaji wa maji katika wilaya ya Nanyumbu ni asilimia 37 ,hivyo mradi huo utakapokamilika utaongeza huduma ya maji safi na salama hadi kufikia asilimia 90 na mradi una nafasi kubwa ya kubadilisha maisha ya wananchi na wilaya ya Nanyumbu.

Alisema,wilaya ya Nanyumbu ina changamoto kubwa ya kimaendeleo kutokana na ukosefu wa maji safi na salama kwani hata wawekezaji wanasita kwenda kuwekeza kwa sababu ya kutokuwa na uhakika wa huduma ya maji safi na salama.

Mkazi wa kijiji cha Masuguru Salum Haule,ameishukuru Serikali kwa uamuzi wa kujenga mradi huo kwani utawezesha kupata huduma ya maji safi na salama na kupata muda wa kujikita

katika shughuli za kiuchumi badala ya kutumia muda mwingi kwenda kutafuta maji.

Post a Comment

Previous Post Next Post