KUSAYA – ASIKITISHWA NA KIWANDA CHA MBOLEA ISACHA CHA MOSHI KUENDESHWA BILA USAJILI WA UBORA

 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa ameshika chupa ya mbolea inayozalishwa na kiwanda cha Isacha Feeder cha Moshi leo alipokagua .Katika ziara hiyo alibaini kuwa kiwanda hicho kinazalisha mbolea ya maji aina ya Booster II ambayo haijasajiliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na  ameagiza mmiliki wa kiwanda hicho aende Dodoma ifikiapo 03 Septemba kujieleza kwanini anaendesha kiwanda bila usajili.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya( kulia) akiongea na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) Dkt.Stephano Ngailo wa kwanza kushoto alipobaini mbolea ya maji isiyo uthibitisho wa ubora toka TBS .Wa kwanza kushoto ni Msimamizi wa kiwanda cha Isacha Feeder -Njoro chaMoshi  Rajab Issa Juma kinachozalisha mbolea hiyo.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya ( kulia) akikagua mgodi wa chokaa (limestone rock)  leo alipotembelea kiwanda cha mbolea cha ABM Jijini Tanga.Kushoto ni Mkurugenzi wa kiwanda hicho Aubray Maimu.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya (kulia) akiangalia eneo panapochimbwa chokaa kilimo katika kiwanda cha mbolea cha ABM Tanga. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania Bw.Saad Kambona.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa anatazama jiwe la chokaa linalotumika kuzalisha mbolea katika kiwanda cha ABM Tanga leo alipotembelea kukagua utendaji kazi wake na kuhamasisha kuongeza uzalishaji ili wakulima wapate mbolea kwa gharama nafuu.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya ( wa tatu toka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Bodi ya Mkonge Tanzania na wanahabari mara baada ya kutembelea bodi hiyo leo jijini Tanga kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya  Waziri Mkuu.
(Picha na habari na Wizara ya Kilimo)

 ……………………………………………………………

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amesikitishwa na kitendo
cha kiwanda cha mbolea za maji cha Isacha Feeders Intertrade cha Moshi
mkoani Kilimanjaro kuzalisha bidhaa za mbolea ambazo hazisajiliwa na
kuthibitishwa ubora wake kwa wakulima.
Akiwa katika ziara ya kukagua viwanda vya mbolea nchini leo 
Katibu Mkuu huyo alijionea bidhaa za mbolea ya maji iitwayo “Booster II”
ikiwa katika ghala la kiwanda cha Isacha Feeder –Njoro Manispaa ya
Moshi na kubaini kuwa haijasajiliwa na mamlaka za uthibiti ubora nchini.
“Sijafurahishwa na utendaji kazi wa kiwanda hiki cha mbolea cha Isacha
Feeders kuona mbolea inayozalishwa haijasajiliwa na Shirika la Viwango
(TBS ) pia haina Barcode hali inayohatarisha mazao ya wakulima na afya
za walaji” alisema Kusaya.
Taarifa ya kiwanda hicho cha mbolea ya maji imeonyesha kilianzishwa
mwaka 2016 kikizalisha mbolea ya maji ambazo zinauzwa kwenye maduka
mbalimbali nchini bila kuwa na usajili wa ubora toka TBS.
Kufuatia hali hiyo, Katibu Mkuu Kusaya ameagiza wamiliki wa kiwanda
hicho kwenda ofisini kwake Dodoma ifikapo tarehe 03 Septemba 2020 ili
kujieleza kwanini serikali isichukue hatua za kukifunga kiwanda hicho hadi
wakamilishe taratibu za usajili ili kulinda wakulima na uharibifu unaoweza
kujitokeza endapo mbolea hiyo ikikosa ubora.
“Ninyi mnazalisha mbolea na kuipeleka kwa wakulima wangu sasa ikitokea
mazao ya wakulima yameharibika na mbolea hii isiyo na uthibitisho wa
ubora nani atalipia gharama hizo?” alihoji Katibu Mkuu Kusaya
Kufuatia hali hiyo Kusaya alitoa maagizo matano kwanza, mmiliki wa
kiwanda hicho cha Isacha kuwasilisha taarifa inayoonyesha tangu mwaka
2016 wamezalisha kiasi gani cha mbolea na wameuza wapi, pili
wawasilishe uthibitisho wa cheti cha kuendesha kiwanda toka BRELA na
Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Agizo la tatu mmiliki wa kiwanda mbolea cha Isacha aeleze kwanini
kiwanda hakina bango la utambulisho na hakijulikani na uongozi wa mkoa

wa Kilimanjaro mahala kilipo na nne kiwanda hicho kiwasilishe taarifa ya
ulipaji kodi serikalini tangu kilipoanza kazi mwaka 2016 hadi sasa.
“Mkija Dodoma nataka mje na taarifa kamili kuhusu uhalali wa kiwanda hiki
kuwa na sifa za kuzalisha mbolea inayokwenda kutumika na wakulima ili
kuishawishi serikali kuwa mnastahili kuendelea ka kazi ” alisisitiza Kusaya.
Kusaya alisema akirejea Dodoma atawaalika Wizara ya Viwanda na
Biashara, Mamlaka ya Mapato (TRA) Shirika la Viwango (TBS), BRELA na
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) wajadili hatua za kuchukua dhidi
ya viwanda ambavyo vinakiuka taratibu za uzalishaji mbolea nchini.
Naye Msimamizi wa kiwanda hicho cha Isacha Feeder -Njoro, Rajab Issa
Juma alisema kiwanda hicho kinazalisha lita 17,000 za mbolea ya maji
(Booster II: Foliar Fertilizer for Use in all Crops) kwa mwaka ambapo lita
moja huuzwa kwa bei ya shilingi 2,000 kwa wakulima.
Awali Katibu Mkuu huyo alitembelea kiwanda cha mbolea ABM cha Tanga
kuona hali ya uzalishaji na kukuta kiwanda hicho kikizalisha chokaa kilimo
chini ya uwezo wake kutokana na changamoto ya mtaji.
Akizungumza na waandishi wa habari kiwandani hapo Mkurugenzi wa
kiwanda hicho Aubray Maimu alisema wanazalisha tani 5,000 za chokaa
kilimo (limestone) kati ya lengo la tani 10,005 kufikia mwaka 2021.
“Mgodi wetu wa Zange Mkulumuzi hapa Kange Tanga una mawe ya
chokaa zaidi ya tani milioni 25 inayotesheleza uzalishaji wa mbolea ya
chokaa kwa wakulima” alisema Maimu.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka Udhibiti wa Mbolea
Tanzania (TFRA) Dkt. Stephano Ngailo amesema mahitaji ya mbolea
nchini ni tani 664,000 wakati uzalishaji katika viwanda vyote 12 umefikia
tani 38,000 pekee kwa mwaka.
Katibu Mkuu Kusaya yuko katika ziara ya kukagua na kujionea hali ilivyo
kwenye viwanda vya mbolea nchini ambapo tayari ametembelea kiwanda
cha Mbolea za Asili cha Guavay cha Dar es Salaam ambapo anatarajia
kutembelea pia mikoa ya Arusha na Manyara
Lengo la ziara hii ni kuhamasisha wawekezaji wa ndani ya nchi na nje
kuanzisha viwanda vya mbolea ili wakulima wapate kwa gharama nafuu na
karibu na mashamba yao badala ya kutegemea mbolea toka nje.

Post a Comment

Previous Post Next Post