SERIKALI, WADAU BEGA KWA BEGA MAPAMBANO YA SARATANI

 

Na WAF – Dar Es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya imendelea kushirikiana na wadau ili kutokomeza ugonjwa wa Saratani nchini ikiwemo utolewaji wa elimu pamoja na kuhimiza upatikanaji wa chanjo ya Saratani ya Mlango wa kizazi kwa wasichana kwa kuwa ugonjwa huo umekua ukiongezeka kila mwaka.

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Oktoba 11, 2024 kwenye ufunguzi wa kitengo cha Saratani kilichopo katika Hospitali ya Shifaa Jijini Dar Es Salaam.

“Ufunguzi wa kituo hiki utaongeza upatikanaji wa huduma za uchunguzi na matibabu ya Saratani hapa nchini kwa kuwa tatizo la ugonjwa huo limekuwa likiongezeka kila mwaka,” amesema Waziri Mhagama

Aidha, Waziri Mhagama amesema takwimu za Saratani kwa mwaka 2022 zinaonesha kuwa, wagonjwa wapya wa Saratani takribani elfu 45 wanagundulika ikiwemo wa Saratani ya mlango wa kizazi asilimia 24.2, Saratani ya tezi dume 10.7%, Saratani ya matiti 10%, Saratni ya koo 7.9% na Saratani ya utumbo mpana asilimia 4.9.

“Saratani hizi zinachukua karibu nusu ya asilimia 42.4 ya wagonjwa wote wa Saratani nchini, na Saratani mbili zinazoathiri zaidi wanawake ni Saratani ya mlango wa kizazi na Saratani ya matiti ambazo zinazachukua theruthi moja ya wagonjwa wote wa Saratani nchini,” amesema Waziri Mhagama

Kufuatia kuongezeka kwa wagonjwa wa Saratani nchini, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu ya afya pamoja na kuimarisha huduma za uchunguzi wa Saratani hususani Saratani ya mlango wa kizazi katika hospitali na vituo vingine vya kutolea huduma za Afya nchini.

“Wajibu wetu kama Serikali ni uthibiti wa ubora na sio udhibiti wa Sekta binafsi kukua, tutaendelea kushirikiana na Sekta binafsi ili kwa pamoja tuweze kutoa huduma iliyo bora na salama kwa wananchi,” amesema Waziri Mhagama.

Ili kuongeza ufanisi katika huduma za uchunguzi, Serikali imeimarisha upatikanaji wa huduma za uchunguzi wa kimaabara pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanywa kwenye huduma za radiolojia kwa kuimarisha upatikanaji wa vipimo vya kisasa ikiwemo CT-Scan 85 katika mikoa yote 26 nchini.      

Post a Comment

Previous Post Next Post