TBS YAKAMATA TANI 20 ZA BIDHAA HAFIFU JIJINI DAR ES SALAAM

 NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV


SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limefanya operesheni maalumu katika Mkoa wa Dar es Salaam na kufanikiwa kukamata tani 20 ya bidhaa hafifu na zisizo na viwango.

Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 11,2024 Jijini Dar es Salaam, Meneja wa TBS Kanda ya Mashariki, Noor Meghji amesema katika operesheni hiyo walijikita kuangalia bidhaa za pombe kali, vipodozi hasa vyenye viambata sumu.

“Kwenye zoezi hilo pia tuliangalia vinywaji vya kusisimua (Energy drink) ambapo baadhi tulizozikamata zilionekana na mapungufu na hazijakidhi vigezo vya ubora unaotakiwa ”. Amesema

Amesema kwa bidhaa ambazo wamezikamata wanatarajia kuziteketeza baada ya siku 14 kwa ajili ya kumpatia nafasi mteja kwa ajili ya kutoa malalamiko anapohisi ameonewa.

Aidha Meghji ameeleza kuwa katika zoezi hilo pia wamefanya ukaguzi wa usajili wa majengo kwa maeneo yanayojihusisha na chakula pamoja na vipodozi ambapo kwa mujibu wa sheria inatakiwa yawe na vibali vya TBS.

"Kuna baadhi ya maduka walikutwa hawana vibali vya TBS, waliandikiwa barua ya onyo nakutakiwa kufuata taratibu wa usajili wa kaduka hayo. "Amesema.

Pamoja na hayo amesisitiza wafanyabiashara kuzingatia utunzaji mzuri wa bidhaa zao kwalengo la kuhakikisha zinasalia na ubora ambao unatakiwa ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kwa mlaji kutumia bidhaa isiyo na ubora.

TBS Kanda ya Mashariki imekuwa ukifanya kaguzi za mara kwa mara katika jiji la Dar es salaam kwani ndio lango kuu la kuingiza bidhaa mbalimbali ili kudhibiti mapema bidhaa zisizo kidhi matakwa ya sheria za viwango zisiingie katika soko la ndani.








Post a Comment

Previous Post Next Post