Kunduchi bomba la Kiswahili linalohitaji maji.

 Na Eben-Ezery Mende

KUNDUCHI ni kilele cha ustaarabu wa Mswahili kwa mujibu wa utafiti wa akiolojia uliofanyika katika pwani zote za Afrika Mashariki

Kwa mujibu wa tafiti hizo, lugha ya Kiswahili chimbuko lake ni eneo la Kunduchi ambalo liko ndani ya Jiji la Kibiashara Dar es salaam.

Mhifadhi wa Mambo ya Kale Kunduchi, Bi. Vicktoria Gilabo Bache anasema eleo hilo lina historia kubwa ihusuyo lugha adhimu ya Kiswahili ambayo inapaswa kukumbukwa na kuhifadhiwa.

Bache anasema mambo yanayobainisha ustaarabu wa Mswahili unatokea kwenye eneo hilo la Kunduchi ni mapambo yaliyopo kwenye magofu ya watu walioishi eneo hilo ambayo yameandikwa kwa lugha ya kiarabu mchanganyiko na Kiswahili.

Lugha hiyo ambayo imeandikwa kwenye magofu ya makaburi na msikiti vilivyopo eneo hilo la kunduchi ni lugha ambayo haipatikani kwenye mazingira yoyote isipokuwa Kunduchi peke yake.

Eneo la kunduchi walizikwa viongozi wa Pwani ya Afrika Mashariki ambao ni Masultani, Masharifu na Sultana.

Kwa tafsiri ya neno Mswahili, ni mbantu  wa Afrika Masharaiki ambaye amepatikana kwa mchanganyiko na Mwarabu, Mhindi, ambao walitokea kusini mwa Somalia, kuelekea kusini mwa Sofala (Msumbiji) katika biashara za wakati huo za masafa marefu.

Maeneo hayo ndiyo yanayobainishwa kuwa yametumika kukieneza Kiswahili na kutokana na utofauti huo wa kimazingira kila eneo lilikuwa na namna yake ya kimatamshi na misamiati.

Koo kuu mawili ndizo zinazobainishwa kwamba ziliishi eneo la Kunduchi ambazo ni Al-Hatmii na Al-Balal.

Katika kutofautisha magofu ya kale maeneo mengine ya kihistoria na yanayopatikana eneo la Kunduchi ni kutokana na Makaburi ya eneo hilo kufunikwa juu ambapo hakuna magofu mengine yaliyofunikwa kwa mfanano huo pwani yote ya Afrika Mashariki.

Bache anasema magofu hayo ya Kunduchi yapo tangu karne ya 13 ambapo magofu yote yaliyofunikwa juu yanafahamika kuwa ni ya Ukoo wa Al-Hatmii ambao chimbuko lake ni Iraq.

Norah Kidodelo ni Mtafiti wa Mambo ya Akiolojia ambaye anasema Kishwahili kilichozaliwa Kunduchi na kupewa hadhi ya Kilele cha Ustaarabu wa Mswahili kinatokana na uhalisia wa makabila ambayo yalikuwa na mwingiliano mkubwa tofauti na kishwahili kilichomea maeneo mengine ya ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki.

Anasema Kiswahili cha Mombasa kimechanganyika na Kiingereza, Kiswahili cha Zanzibar pia kina mchanganyiko wa maneno ya Kiingereza na misamiati ya tofauti ikilinganishwa na Kiswahili cha Kunduchi.

Kwa mujibu wa Kidodelo lugha ya Kiswahili katika maeneo ya Pwani ya Mashariki imetofautiana kutokana na utofauti wa tawala za karne ya 13.

Anasema Kiswahili kilichotumika Kunduchi ni tofauti na Kiswahili kilichotumika maeneo yote ya Pwani ya Afrika Mashariki kwani kilikuwa na maneno na lafudhi maalumu kutokana na mukhtadha wa eneo hilo.

Kidodelo anasema wakazi wa Kunduchi wanatumia lugha ya Kiswahili katika mawasiliano yao ya kila siku na kinaweza kuwa na athari za lugha nyingine kutokana na lafudhi, misamiati maalumu na hivyo kuwa na utofauti na ulinganifu.

Lafudhi: Inaelezwa kuwa Kunduchi lafudhi ya watu wa eneo hilo inaweza kuwa na athari za kikabila na mikoa mingine  tofauti na maeneo kama Zanzibar na Mombasa ambapo kuna lafudhi na matamshi maalumu.

Misamiati: Kwa mujibu wa Kidodelo, Kunduchi kuna maneno ya kisasa yanayoweza kuingizwa kutoka kwenye lugha nyingine kama vile kiingereza na lugha za kikabila na hilo linaweza kuwa tofauti na Kiswahili cha jadi kinachozungumzwa maeneo ya mbali na mjini.

Mukhtadha wa Kijamii: Mwana Akiolojia, Kidodelo anasema Kiswahili kinatumika katika mazingira tofauti kama vile, masoko, shuleni, na kwenye shughuli za kijamii, hali inayochangia mabadiliko katika matumizi ya lugha.

Adhari za kijamii na kiuchumi: Kidodelo anabainisha kwamba, maeneo kama Nairobi Kiswahili kinachanganyika na kiingereza wakati maneno mengine yanaweza kuwa na mtindo wa Kiswahili kilichotumiwa kwa ufasaha Zaidi bila kuingilia lugha nyingine.

Kuhusu viongozi wakuu wa Tanganyika wakati huo na sasa Tanzania akiwemo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wanaelezwa kwamba walipigania lugha hiyo ambayo leo inatambulika kama lugha kuu ya Afrika na kutambulika kimataifa kwa kupewa siku maalumu ya Kiswahili ambayo ni Julai 7.

Kidodelo anasema, Mwl. Nyerere alikuwa anatembelea maeneo ya kumbukumbu ya magofu ya kale Kunduchi kwa lengo kuu la kukuza utamaduni wa Kiswahili, kukienzi na kuhamasisha Watanzania kuitumia lugha hiyo kwa ufasaha kwani ni silaha iliyorahisisha mawasiliano wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika.

Aidha Kidodelo anasema wakati wa uongozi wa Rais Ali Hasan Mwinyi alichangia kukuza lugha ya Kiswahili kwa kuhamasisha uongozi kutumia lugha hiyo katika maeneo yao ya utumishi.

Aliyekuwa Waziri Mkuu, Rashidi Mfaume Kawawa naye anaelezwa kuwa alihusika kwa kiasi kikubwa kuhakikisha lugha ya Kiswahili inazingatiwa katika matyumizi ya kawaida.

Kawawa ambaye katuika utumishi wake aliwahi kuwa mlezi wa taasisi ya Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA) alikuwa kiongozi wa kuigwa katika kupigania lugha hiyo ambayo leo ni zao miongoni mwa mazao ya Utalii nchini.

Kidodelo anasema Kunduchi limekuwa eneo linalotumiwa kwa Matamasha na shughuli za kitamaduni zinazohusisha Kiswahili ambapo viongozi mbalimbali huhudhuria na kuwahamasisha wananchi kujihusisha na urithi wa lugha na utamaduni wao.

Yapo mataifa ambayo yamekuwa kinara kwa kutembelea eneo la Kunduchi kujionea historia ya magofu ya eneo hilo ambayo ni India, Uingereza, Australia, Afrika ya Kusini, Inan, Iraq, Kenya, Congo na Uganda.

Ushauri.

Kidodelo anasema Serikali inapaswa kuandaa mikakati ya uhifadhi wa makaburi ya Kiswahili ya Kunduchi ambayo ni tathmini na uandishi wa historia kwa kufanya utafiti wa kina ili kuandika hali ya sasa ya makaburi ikiwa ni pamoja na uadilifu wa muundo, muundo wa vifaa na athari za mazingira.

Aidha anashauri ufanyike utafiti wa kihistoria kwa kukusanya taarifa za kihistoria na hadithi za mukhtadha zinazohusiana na makabuiri ili kuelewa umuhimu wao wa kitamaduni na mukhtadha wa kihistoria.

Kuhusu uhifadhi wa muundo anasema, inatakiwa ufanyike utekelezaji wa matengenezo ya mara kwa mara ili kushughulikia matatizo madogo kabla ya kuwa makubwa. Na kwa kuzingatia njia ya mbinu za ukarabati vinatakiwa vitumike vifaa na mbinu za jadi za ukarabati ili kuhifadhi uhalisia wa historia kwa kuepuka kutumia vifaa vya kisasa ambavyo vinaweza kubadilisha mwonekano wa asili.

Fauka ya halo, anasema usimamizi wa mazingira ni muhimu ukazingatiwa kwa kudhibiti unyevu na joto katika maeneo ya makaburi ili kuzuia uharibifu kutokana na sababu za mazingira, pia iwekwe mifumo ya mifereji ili kudhibiti mvua na kuzuia mmomonyoko au uharibifu wa maji kwenye muundo.

Kipengele cha ushirikishwaji wa jamii pia kinaelezwa kuwa na umuhimu mkubwa katika kutunza eneo la magofu ya kale Kunduchi ili kuhakikisha shughuli za uhifadhi zinahusiana na tamaduni na zinaungwa mkono na wale walio na hisa katika maeneo hayo.

Pia Kidodelo anashauri itengenezwe programu za elimu ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa makaburi na kuhamasisha utunzaji wa ndani.

Mtafiti, Kidodelo anasisitiza kwamba mfumo wa kisheria na sera vitawezesha kuliweka eneo la kihistoria la Kunduchi kwenye hali nzuri ambayo itadumu kwa kuvutia watalii kutembelea eneo hilo.

Anasema, sharia za ulinzi zinatakiwa kuandaliwa ili zitumike kulinda makaburi ambapo itasaidia kuzuia uharibufu na mabadiliko yasiyokuwa na idhini. Pia itasaidia kuhakikisha kuwa makaburi yanapewa ulinziwa kisheria dhidi ya vitendo vya uharibifu.

Ushauri mwingine anaoutoa, Kidodelo ni kuwepo mpango wa usimamizi unaobainishamalengo ya uhifadhi, mikakati na majukumu na mipango hiyo inapaswa kujumuisha hatua za kutekeleza uhifadhi kufuatilia hali ya makaburi na kushirikisha wadau mbalimbali katika mchakato.

Ushauri mwingine ni Uhamasishaji wa Umma ambapo, Kidodelo anashauri uwepo uhamasishaji wa umma kuhusu umuhimu wa sharia za ulinzi wa makaburi ili kuongeza uelewa na ushirikishwaji wa jamii na wadau katika juhudi za uhifadhi.

Mwisho anashauri uwepo ushirikiano na Serikali kwa kufanya kazi na mamlaka za Serikali za mitaa na kitaifa ili kuhakikisha kuwa sharia zinatekelezwa ipaswavyo na rasilimali zinapatikana kwa ajili ya uhifadhi.

Kidodelo anatamatisha kwa ushauri kwamba Kivutio cha historia ya magofu ya Kunduchi kinapaswa kuboreshwa miundombinu kama barabara, kuongeza vivutio mfano michezo ya watoto na utafiti Zaidi kuyahusu magofu.



Post a Comment

Previous Post Next Post