TANZANIA YAZIDI KUPAA SEKTA YA UTALII

 Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma


Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika sekta ya utalii kwa kuwa na kiwango kikubwa cha watalii wanaotembelea vivutio mbalimbali kulinganisha na nchi nyingine Barani Afrika kwa mujibu wa ripoti ya nusu mwaka ya takwimu za utalii ya shirika la utalii duniani (UN Tourism Barometer Report) katika kipindi cha kuanzia mwezi januari hadi julai, 2024.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana wakati wa Mkuatano wake na vyombo vya habari uliofanyika Ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

Ameeleza kwamba Tanzania imekuwa nchi ya sita (6) duniani kwa kuwa na ongezeko la asilimia 49 la watalii ikitanguliwa na Qatar. Kwa takwimu hizo Tanzania imepanda hadi nafasi 2 juu ambapo kwa kipindi kama hicho, mwaka jana ilishika nafasi ya nane (8) duniani ikiwa na ongezeko la asilimia 19.

Waziri Chana alisema,”Ukuaji wa sekta ya utalii unatokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amekuwa mstari wa mbele kwa kuleta mageuzi makubwa katika utangazaji utalii kupitia Programu ya Tanzania-The Royal Tour na Amazing Tanzania halikadhalika kuendelea kuboresha miundombinu ya utalii nchini.”

Amefafanua kwamba, Juhudi hizo zimesaidia Wizara ya Maliasili na Utalii kupokea tuzo nne (4) za World Travel Awards kwa mwaka 2024 katika vipengele vya: Kivutio Bora cha Utalii Afrika (African Leading Tourism Attraction 2024) – Mlima Kilimanjaro; Hifadhi Bora ya Taifa Afrika (Africa’s Leading National Park 2024) – Hifadhi ya Taifa Serengeti; Kituo Bora cha Utalii Afrika (African’s Leading Destination) – Tanzania; Bodi Bora ya Utalii Afrika (African Leading Tourism Attraction 2024) – Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Aidha ameipongeza Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kwa kufanikisha Visiwa vya Zanzibar kushinda tuzo ya eneo maridhawa kwa Matukio na Matamasha (African’s Leading Festivals and Events Destination 2024).

Pia Wakala wa Biashara za Utalii nchini ambao wameshinda tuzo hizo katika vipengele mbalimbali kutokana na juhudi zao za kutoa huduma bora katika sekta ya utalii. Napenda kuwapongeza: Gran Meliá Arusha, Twiga Tours, Lamai Serengeti, Kuro Tarangire, Altezza Travel, Satguru Travel Tanzania, Skylink Travel & Tours na Gosheni Safaris.

Amebainisha kwamba, “ Tuzo hizi zinaitangaza Tanzania kimataifa kama kituo bora cha utalii barani Afrika ambapo zitawezesha kuvutia watalii zaidi, hususan kutoka masoko ya utalii ya kimkakati nayanayochipukia.”





Post a Comment

Previous Post Next Post