DKT. BITEKO AKARIBISHA WAWEKEZAJI SEKTA YA NISHATI

 

*Ashiriki Wiki ya Kimataifa ya Nishati Singapore, Aeleza Mafanikio ya Sekta hiyo Tanzania

 *Ataja Mkakati wa Serikali Kuimarisha Sekta ya Nishati

 *Aeleza Namna Tanzania Inavyojiandaa Kuuza Umeme nchi Jirani na Uwepo wa Soko la Uhakika

 *Abainisha Umuhimu wa Sekta Binafsi kushiriki Mipango ya Maendeleo

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali inawakaribisha wawekezaji katika sekta ya nishati ili kuongeza kasi ya uzalishaji, usambazaji na uunganishaji wa wateja katika Sekta ya Nishati nchini.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Oktoba 21, 2024 nchini Singapore wakati akishiriki mjadala kuhusu nishati ambao ulishirikisha Waziri wa Madini na Nishati wa Cambodia, Mhe. Keo Rottanak na Waziri wa Maliasili kutoka New Zeland Mhe. Shane Jones katika ufunguzi wa Wiki ya Kimataifa ya Nishati nchini Singapore.

“ Serikali haziwezi kufanya kila kitu zenyewe hivyo ni muhimu kushirikiana na sekta binafsi. Sisi Tanzania tunawaalika sekta binafsi ili kuwekeza katika sekta ya nishati kwa ajili ya kuimarisha uzalishaji, upatikanaji na usambazaji nishati na kuboresha maisha ya watu kwa ujumla,” amesema Dkt. Biteko.

Akizungunzia, ajenda ya nishati safi ya kupikia nchini amesema kuwa ni matokeo ya utafiti uliofanywa na kubaini kuwa idadi kubwa ya Watanzania wanatumia kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia hali inayosababisha magonjwa ya mfumo wa upumuaji na uharibifu wa mazingira.

Ili kupunguza athari hizo, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali imeandaa mkakati unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

“ Serikali imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na kuhakikisha nishati safi inapatikana kwa urahisi na bei nafuu na hivyo tunawakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza katika hili kwa sababu soko lipo,” amesema Dkt. Biteko.

Aidha, Dkt. Biteko ametaja miradi mbalimbali inayofanywa na Serikali ikiwemo mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2115 ambao amesema kukamilika kwake kutaongeza ziada ya umeme nchini.

“ Serikali inaendeleza vyanzo vipya vya nishati mfano umeme wa jua, upepo na gesi, aidha kwa sasa asilimia 51 ya umeme unazalishwa kwa maji. Tanzania tumeendelea na maandalizi ya kuziuzia umeme nchi za Kenya, Rwanda, Burundi na sasa tunaendelea na mradi kwa ajili ya kuunganisha na nchi ya Zambia, kupitia Umoja wa Mauzio ya Umeme wa pamoja katika nchi za Afrika Mashiriki na Jumuiya za Kusini mwa Afrika (SADC) tuna soko la uhakika na hivyo tunawakaribisha wawekezaji kuja kushirikiana nasi,” amesisitiza Dkt. Biteko.

Naye, Waziri wa Madini na Nishati kutoka Cambodia, Mhe. Keo Rottanak amesema kuwa mwaka 1998 nchi yake ilifanya mageuzi makubwa katika sekta ya nishati na kuwa sasa asilimia 99 ya vijiji vina umeme.

“ Tutahakikisha tunafikisha umeme katika nyumba za watu na malengo yetu ni ifikapo mwaka 2030 tunazalisha umeme kwa nguvu ya jua kama mbadala wa umeme unaozalishwa kwa nguvu yamaji,” amesema Mhe. Rottanak.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na kutoka nchini New Zeland, Mhe. Shane Jones amesema kuwa nchi yake imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya kusambaza umeme na kuwa inajikita katika kuwekeza katika vyanzo mbadala vya kuzalisha nishati.

Awali akifungua mkutano huo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Singapore Mhe. Gan Kim Yong amesema kuwa mahitaji ya nishati duniani yanazidi kuongezeka siku hadi siku hivyo nchi zinapaswa kubuni vyanzo mbadala na kupunguza madhara yatokanayo na gesi ya ukaa ifikapo mwaka 2050.

amesema nchi yake imeongeza vyanzo mbadala vya nishati na kuiobgeza kuwa kwa sasa inajielekeza katika matumizi ya Hydrojen “ Kwa sasa tuko kwenye mkakati wa kuzalisha umeme kwa kutumia hydrojen na nyuklia ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuongezeka kwa ushiriki wa Kampuni za Google na Amazon ambazo zimeonesha nia ya kuwekeza kwenye miradi ya nishati jadidifu.” Amesema Mhe. Kim Yong.

Aidha,katika mkutano huo pia umefanyika uzinduzi wa tawi la ofisi ya kanda ya Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA) nchini Singapore.

   

Post a Comment

Previous Post Next Post