WAZIRI SIMBACHAWENE: UJENZI WA MAHAKAMA KATIKA KIJIJI CHA KINUSI UTACHAGIZA UTAWALA BORA KATIKA JAMII

 Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi mwa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, Mhe, George Simbachawene amesema ujenzi wa mradi wa Mahakama ya Mwanzo ya Kisasa  katika Kijiji cha Kinusi  unaweka historia kwani sehemu inapojengwa ni eneo gumu kufikika hivyo itasaidia kuchagiza utawala bora kwa wananchi wa Jimbo la Kibakwe kwa ujumla. 

  Ametoa kauli hiyo leo  katika Kijiji cha Kinusi kilichopo Kata ya Ipera,  Halmashauri ya Wilaya ya  Mpwapwa  jijni Dodoma wakati wa tukio la  kukakabidhi eneo hilo  la ujenzi wa Mahakama  kwa Mkandarasi.  

Amesema mradi huo wa ujenzi wa  Mahakama utakaogharimu shilingi Bilioni 1.1 hadi kukamilika kwake  umekuja kwa wakati  muafaka kwani  wananchi  hawatalazimika  kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kwenda  kutafuta haki zao Wilayani Mpwapwa. 

Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa  ujenzi wa jengo hilo unarudisha historia ya eneo hilo la Ipera kwani  miaka ya 1952 kulijengwa Mahakama na Waingereza iliyoanza kufanya kazi huku aliyekuwa  Chifu wa eneo hilo,  Chifu Zaina Sechamule  alitumika kama Hakimu.

" Kihistoria eneo hilo linajulikana  kwa jina la Kwilondoo ndiko eneo ambako kulikuwa kunapatikana haki na ndilo  eneo  alikokuwa akiishi Chifu na  huyu alikuwa ni Chifu mwanamke, hivyo leo ni siku ya kihistoria ya kukabidhi eneo la ujenzi wa mahakama ya kisasa’’ amesisitiza Mhe. Simbachawene. 

Amesema ujio wa mahakama hiyo itasaidia kutoa haki  kwa zaidi ya wananchi wa   Kata sita zilizopo katika eneo hilo huku akizitaja hata  zile Kata za jirani za  Wilaya ya Kilosa, Mkoani Morogoro zitanufaika pia

Awali  Mtendaji Mkuu wa Mahakama  ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema ujenzi wa Mahakama hiyo utagharimu Sh. Bilioni 1.1  na utachukua muda wa miezi nane hadi kukamilika kwake. 

Amesema ujenzi huo utaleta chachu  katika maendeleo ya eneo hilo huku akisisitiza kuwa Mradi huo ni wa kihistoria kwa sababu Kinusi ni miongoni mwa maeneo ambayo  wameyabainisha kuwa  ni magumu kufikika.

 " Naomba nimshukuru sana Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na msukumo mkubwa anaouweka kwenye mahakama hauelezeki  kwa vile Mimi ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Mimi ndio Afisa Masuhuli ninajua ninachokimaanisha" amesisitiza Prof.Elisante

Naye, Mkandarasi wa Jengo hilo,  Audax Contractors mara baada ya  kukabidhiwa eneo hilo ameahidi kukabidhi jengo hilo ndani ya muda  huku akikisitiza ataheshimu makubaliano ya mkataba na kuhakikisha kuwa atazingatia  masharti yote katika ujenzi wa mradi huo.




Post a Comment

Previous Post Next Post