PROFESA MKENDA AWASHAURI WACHUMI KUFANYA TAFITI ZITAKAZOISAIDIA SERIKALI


NA Mwandishi Wetu


WACHUMI nchini wameshauriwa kufanya tafiti kwa ajili ya kuangalia namna ya kutatua changamoto zinazoikabili nchi kulingana na mazingira yaliyopo ili kuleta tija kwa Serikali kupiga hatua stahiki hususan katika kuwasaidia vijana kuwa na uwezo wa kujiajiri au kuajiariwa

Hayo yatatokana kuwa na uchumi imara utakaosaidia vijana kuwa na uwezo wa kujiajiri ama kuajiriwa kutokana na kuzalishwa ajira lukuki, hivyo wachumi wanapaswa kuisaidia Serikali kutatua changamoto zinazoikabili katika sekta ya uchumi.

Hayo yamebainishwa leo, Julai 12, 2024 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda wakati akifungua Kongamano la Pili la mwaka 2024 la Uchumi (EST) la Jumuia la Wachumi Tanzania.

 

Profesa Mkenda ambaye alimwakilisha Makamu wa Rais, Dkt Philip Mpango ambapo alisistiza kuwa ikiwa wachumi hao watafanya tafiti zao kulingana na mazingira ya nchi na kuishauri Serikali namna ya kutatua changamoto za kiuchumi kwa maendeleo ya taifa.

“Nafasi ya wachumi ni kuhakikisha wanachambua masula mbalimbali ya kiuchumi kitaalamu na kuibua changamoto zilizopo na kuipa Serikali njia stahiki ya kufanya kwa lengo la kupata matokeo mazuri,” amesema.

 

Amefafanua kuwa mageuzi ya uchumi yatachochewa na tafiti nzuri zitakazofanywa na wachumi zitakazosaidia kuongeza ajira kwa kundi la vijana ambalo linahitaji kusaidiwa ili kuwafikisha katika matarajio yao kwa kushiriki katika uzalishaji mali jambo litakalofanikisha ukuaji wa uchumi.

 

Amesema hadi sasa Serikali imefanikisha kwa asilimia kutekeleza nyanja mbalimbali za kiuchumi na kuleta mageuzi makubwa ya kwenye sekta ya elimu kwa kuboresha miundombinu inayosaidia kupatikana kwa elimu bora kwa Watanzania na siku zijazo ni dhahiri itachagiza kuongezeka kwa wataalamu wa uchumi nchini.

 

Naye, Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Wachumi Tanzania, Dkt Tausi Kida, amesema kongamano hilo linaambatana na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa jumuiya utakatoa fursa ya kuchaguliwa kwa safu mpya ya uongozi.

 

"Kwa siku ya leo kutakuwa na mada mbalimbali zitakazojadili kwa kina kuhusu mwenendo wa uchumi na baada ya kuhitimisha mijadala mchakato unaofuata utakuwa ni wa kuchagua, Mwenyekiti na Makamu wake na wajumbe,” amesema.

Post a Comment

Previous Post Next Post