Wakazi wa Kata ya Sinza, Wilaya ya Kinondoni wametolewa hofu ya upatikanaji wa huduma ya maji kwenye maeneo yao kufuatia jitihada kubwa zinazotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) za kufikisha huduma ya maji kwa uhakika.
Diwani Kata ya Sinza Ndugu Raphaeli Awino ameeleza hayo wakati alipotembelea mradi wa kuongeza huduma ya maji ambao umeanza kutekelezwa na Mamlaka kwa lengo la kuondoa changamoto ya uhaba wa maji Sinza.
Amesema kuwa eneo la Sinza hususani mtaa wa Sinza C na D limekuwa kwenye changamoto ya upatikanaji mdogo wa maji kwa muda sasa kutokana na maji kuwa na msukumo mdogo, lakini kutokana na jitihada zinazoendelea kutekelezwa na DAWASA, ikiwemo za mradi wa kuongeza maji Sinza C na D, hali hiyo itaenda kuisha karibuni.
“Leo nimetembelea na kuona kazi kubwa inayofanywa na DAWASA, naishukuru Serikali yetu na nimpongeze na kumshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utayari wake wa kuelekeza fedha nyingi kwenye miradi ya huduma ya majisafi kwa wananchi wake, hii ishara ya upendo kwa watanzania wote,” ameeleza Ndugu Raphaeli.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huu Meneja wa Mkoa wa kihuduma DAWASA Magomeni, Bi Julieth John amesema kuwa mradi huu unatekelezwa kwa lengo la kuongeza msukumo wa maji kwenye eneo la Sinza C na D ambalo linapata maji wa msukumo mdogo.
“Hivyo kutokana na hali hiyo, kazi kubwa imeanza kufanyika inayohusisha uchimbaji na ulazaji wa mabomba ya inchi 6 kwenye eneo la umbali wa kilomita 1 na mita 30, kuanzia eneo la ubungo maji hadi njia panda ya kuingia Mawasiliano, ambapo litaungwa kwenye mtandao mwingine wa bomba la inchi 6 kwa lengo la kuongeza msukumo wa maji kwenye eneo la Sinza,” amesema.
Ameongeza kuwa kwa sasa wanaongeza upatikanaji wa maji kutoka kwenye Mtambo wa Ruvu Juu ili kuongezea kiasi cha maji kinachotoka kwenye Mtambo wa Ruvu chini.
“Kazi hii inatarajiwa kukamilika mapema mwezi huu na kuwezesha wananchi wote wa Sinza kufurahia huduma, hivyo niwape Imani ya kupata maji kwa wingi katika kipindi kifupi,” ameeleza Bi Julieth.