TFRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yaweka mikakati usambazaji mbolea msimu wa kilimo 2024/ 2025

Na Mwandishi Wetu,

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, imekutana na wadau wa Mbolea wa Mkoa wa Katavi kwa lengo la kufanya Tathmini ya hali ya usambazaji wa Mbolea Msimu wa kilimo 2023/2024 na kufanya maandalizi ya msimu mpya wa 2024/2025.

Kikao hicho kilichofanyika mwishoni mwa wiki  kilihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa  TFRA, Joel Laurent kiliambatana na mafunzo kwa wafanyabiashara 52  waliohitimu mafunzo ya biashara ya mbolea na ambapo aliwatunukia vyeti. 

Ameongeza kuwa, mafunzo hayo ni chachu kwa wafanyabiashara kuweza kutoa elimu/ufafanuzi kwa wakulima juu ya matumizi sahihi ya mbolea na hivyo kuwawezesha wakulima kuongeza tija kwenye uzalishaji.

Laurent ameeleza umuhimu wa wakulima kuzingatia suala la kupima afya ya udongo kupitia maafisa ugani waliopo katika kata zao  kwa kutumia vipima udongo vilivyotolewa na Serikali ili kutambua upungufu wa virutubisho vilivyopo katika udongo wanaoulima na kutumia mbolea sahihi. 

Ameeleza kuwa, msimu wa kilimo 2024/2025 Serikali itatoa vishikwambi vitakavyosaidia zoezi la usajili wa wakulima kwa kuchukua alama za vidole, picha na majira ya nukta (GPS Coordinates) kulingana na ukubwa wa shamba na kutoa wito kwa wakulima kujitokeza kujiandikisha ili kutumia fursa ya ruzuku inayotolewa na Serikali.

Amesema, Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi cha misimu miwili 2022/23 na 2023/24 imetoa mbolea za ruzuku kwa wakulima kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji kwa mkulima ili azalishe kwa tija, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza malighafi za viwanda.

Aidha, amewahakikishia wadau wa mbolea kuwa Serikali itaendelea kutoa Ruzuku ya Mbolea katika Msimu wa 2024/2025 na mbolea zote zitakuwa katika mfumo wa ruzuku.

Pamoja na hayo,  amezielekeza kampuni za mbolea za  ETG, OCP, Africian, Minjingu, TFC, Yara na nyinginezo kuhakikisha mbolea zinawafikia wakulima kwa wakati na kuwa na mawakala wadogo wadogo watakao fikisha mbolea hizo  katika ngazi za Wilaya hadi Kata ili kuwawezesha wakulima kununua mbolea mapema.



Post a Comment

Previous Post Next Post