TBS Yatoa Neno Kuelekea Siku Ya Chakula Salama Duniani

 NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV


Katika kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Chakula Salama Duniani, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limewataka wananchi kuhakikisha chakula kinakuwa salama kabla ya matumizi ili kuweza kulinda afya zao.

Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo ambayo yanatarajiwa kufanyika Juni 7,2024 inasema” Chakula Salama Jiandae kwa Usiyoyatarajia” iliyobeba dhima kubwa yenye lengo la kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa chakula salama.

Akizungumza na waandishi wa habari leo June 4,2024 Jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja wa Kitengo Cha Kufanya Tathmini ya Vihatarishi Vya Chakula (TBS), Dkt.Ashura Katunzi amesema kuwa chakula kisipokuwa salama kinaweza kusababisha magonjwa yanayoambukiza ikiwemo kipindupindu.

“Watanzania wanatakiwa kuwa makini katika kuhakikisha chakula kinakuwa salama ili kukinga miili yao na vimelea sugu kwani tunaweza kurudisha nyuma nguvu kazi na kupelekea uchumi kushuka”. Amesema Katunzi.

Aidha amesema kila mtu anawajibu wa kuhakikisha  anatumia chakula salama kwani chakula salama ni jukumu la kila mmoja wetu.

Pamoja na hayo amesema kuelekea maadhimisho hayo wanatarajia kuwa na mijadala mbalimbali ambayo itakuwa inahusisha mada kuhusu chakula salama kwa jamii ya watanzania.

Post a Comment

Previous Post Next Post