Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah (watatu kushoto) akimkabidhi Tuzo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ACTIVE MAMA, Bi. Ernesta Mwenda (watatu kulia) katika Maadhimisho ya Siku ya Miliki Ubunifu Duniani iliyofanyika leo April 28,2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JINCC) Jijini Dar es Salaam. (wa pili kushoto) ni, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Gofrey Nyaisa.
Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah (watatu kushoto) akimkabidhi Tuzo mmoja wa Wabunifu walioshiriki katika Maadhimisho hayo, Mkuu wa Kitengo cha Sheria, Taasisi ya Sheria Kiganjani Neema Magimba (watatu kulia).
Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya BRELA Bi. Judithi Francis Kadege (kulia) akiungana na Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah (watatu kushoto) pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Gofrey Nyaisa, (wapili kushoto) kupiga makofi kuwapongeza washiriki waliopata Tuzo katika hafla hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt Hashil Abdallah akizungumza alipokuwa akitoa Hotuba yake kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Ashatu Kijaji katika Maadhimisho hayo.
Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Gofrey Nyaisa, akizungumza alipokuwa akitoa salamu za utangulizi katika Maadhimisho yao yaliyofanyika leo April 28, Jijini Dar es salaam.
Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.
Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt Hashil Abdallah amesema Wizara hiyo ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuwepo kwa Sera ya Taifa ya Miliki Ubunifu zitakazosaidia kuimarisha na kuongeza maeneo mapya ya ulinzi wa Miliki Ubunifu nchini.
Dkt. Hashil ametoa kauli hiyo katika kwa niaba ya Waziri mwenye dhamana na wizara hiyo Dkt. Ashatu Kijaji maadhimisho ya siku ya Miliki Ubunifu Duniani iliyofanyika leo April 28,2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JINCC) Jijini Dar es Salaam.
Amesema kukamilika kwa sera hiyo kutasaidia kutoa miongozo itakayoimarisha miundo ya Kisheria na Kitaasisi katika eneo la Miliki Ubunifu kutoa urahisi wa usimamiaji na uratibu wa Miliki Ubunifu nchini.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali hususani utekelezaji wa Malengo ya Mpango wa kuboresha mazingira ya Biashara lengo kubwa likiwa kuweka Mazingira Bora na wezeshi kwenye Sekta zote ikiwa pamoja na eneo la Miliki Ubunifu ambalo linakuwa kwa kasi Duniani”
“Maandalizi ya Sera hii yalihusisha Sekta za Uma na Binafsi na Baadhi yenu mmeshiriki katika midahalo mbalimbali ambayo tunakwenda kuikamilisha sasa”
Ameongeza kuwa Serikali pia imeanzisha mchakato wa kufanya mapitio ya sheria mbalimbali ya Miliki Ubunifu kwa lengo la kuziboresha ili ziweze kwenda na wakati na kutoa urahisi wa usimamiaji na uratibu wa Miliki Ubunifu nchini.
“Ni wazi kuwa kwa sasa zipo baadhi ya Sheria ya Miliki Ubunifu ambazo ni za muda mrefu,na pia yapo baadhi ya maeneo mengine ambayo hayalindwi kisheria, ukizingatia kuna badhi ya Sheria ya Miliki Ubunifu ni za muda mrefu na kuna baadhi yamaeneo mengine bado hayalindwi kisheria. Serikali itazipitia upya Sheria zote” ameongeza Dkt. Ashil.
Aidha amewapongeza Wabunifu wote waliopata Tuzo katika Hafla hiyo na kusema kuwa Tuzo hizo zikawe chachu ya kuongeza juhudi katika Shughuli zao na kuendelea kuwa wabunifu wa mambo mengi zaidi zitakazoleta tija kwa jamii na Taifa kwa Ujumla.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Gofrey Nyaisa amesema kuwa BRELA wameweka mikakati mizuri ya kuboresha huduma wanazotoa na kuzisimamia ili kuvutia zaidi wabunifu na kazi zaidi wanazo zibuni ili kuongeza idadi ya Sajili za kazi zao na kuhakikisha wabunifu hao wanapata manufaa ya kazi zao.
Maadhimisho hayo ya Siku ya Miliki Ubunifu Duniani yalihusisha wadau mbalimbali kutoka Serikali na Sekta Binafsi ambapo mada mbalimbali zilitoletwa.
Kauli mbiu ya Siku ya Miliki Ubunifu kwa Mwaka huu ni, “Wanawake na Miliki Ubunifu: kuongeza kasi ya Ubunifu katika Biashara” lengo la Kauli Mbiu hii ni kutambua mchango wa Wabunifu wanawake katika kukuza Biashara na nafasi yao katika ukuaji wa uchumi nchini.
PICHA MBALIMBALI ZA WADAU WALIOHUDHURIA KATIKA MAADHIMISHO HAYO.