WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAPONGEZWA UWEKEZAJI HIFADHI YA TAIFA KISIWA CHA RUBONDO, NA BURIGI-CHATO

 Na. Catherine Mbena/RUBONDO


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma imeipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo na Burigi-Chato ambapo kwa Hifadhi ya Taifa Rubondo kunafanyika ujenzi wa majengo matatu ya malazi ya wageni mashuhuri katika eneo la Kageya, na katika Hifadhi ya Taifa Burigi -Chato kunafanyika ujenzi wa jengo la kutolea Taarifa za Hifadhi kwa watalii katika Lango la Meja Jenerali (Mstaafu) Salum Kijuu katika eneo la Katete, miradi ambayo inagharamiwa na serikali kupitia fedha za Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO -19

Akizungumza baada ya ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi hiyo leo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma ,Mhe.Jerry Silaa (Mb) alisema

“Tumekuja huku kwa maana ya kuona na tunaposema kwenye kamati tuseme mambo ambayo tumeyaona wenyewe kwa macho, uwekezaji huu katika Hifadhi hizi ni wakupongezwa mno, serikali na wizara kwa ujumla, tunaamini lile lengo la kufikia watalii million tano na mapato ya dola billioni sita ifikapo 2025 inakwenda kutimia” alisema Mhe. Silaa

Awali, akiwakaribisha Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini TANAPA, Jenerali(Mstaafu) George Waitara alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuelekeza fedha hizo katika kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii nchini.

Waitara aliongeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) lilipatiwa fedha kiasi cha shillingi Billioni 46 ili kutekeleza miradi mbalimbali katika Hifadhi ya Taifa Tarangire, Kilimanjaro, Mkomazi, Serengeti, Nyerere, Burigi-Chato, Katavi, Gombe, na Saadani ambapo hadi sasa shirika limepokea fedha zote sawa na asilimia 100 ya fedha zote ambapo Hifadhi ya Taifa Burigi- Chato Ilitengewa kiasi cha shillingi billioni 1.1 na Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo kiasi cha shillingi million 545 kilitengwa ili kutekeleza miradi hiyo.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma imefanya ziara katika Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo na Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato na kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya fedha za UVIKO -19 inayoendelea kutekelezwa katika Hifadhi hizo.



Post a Comment

Previous Post Next Post