MGANGA MFAWIDHI HOSPITALI YA WILAYA LINDI AISHUKURU SERIKALI KWA UMEME WA REA

 

Veronica Simba – Lindi

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Lindi, Dkt. Kassanga Benito, ameishukuru Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kubuni na kuendelea kutekeleza miradi ya umeme vijijini ambayo imewezesha uboreshaji wa huduma katika sekta mbalimbali, ikiwemo afya.

Aliyasema hayo Januari 27, 2023 wakati akizungumza na Ujumbe kutoka REA ulioongozwa na Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Oswald Urassa, ukiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini.

Akieleza furaha yake, Dkt. Benito alisema Hospitali hiyo ya Wilaya ya Lindi ni miongoni mwa wanufaika wa umeme vijijini na kwamba nishati hiyo imewezesha utoaji huduma zote muhimu za afya kwa wananchi kwa ufanisi jambo ambalo lisingewezekana pasipo kuwa na umeme.

“Tunatoa huduma karibu zote kubwa za afya na kwa sasa tumeanzisha kambi ya upasuaji hospitalini hapa huku tukijipanga kuendelea kuongeza huduma nyingine mbalimbali,” amefafanua Mganga Mfawidhi.

Aidha, alitaja manufaa mengine ya uwepo wa umeme hospitalini hapo kuwa ni pamoja na kuwezesha kuhifadhi damu huduma ambayo isingewezekana pasipo umeme.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi alimhakikishia Dkt. Benito kuwa Bodi ya Nishati Vijijini itaendelea kuisimamia REA ipasavyo ili kuhakikisha miradi ya nishati vijijini inaendelea kutekelezwa kwa tija nchini kote kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Hospitali ya Wilaya ya Lindi ilianza kutoa huduma za afya kwa wananchi mwaka 2020. Kabla ya hapo, wnanchi walikuwa wakipata huduma hizo katika hospitali ya Nyangao.


Post a Comment

Previous Post Next Post