REA YAZINDUA MRADI WA KUSAMBAZA UMEME MAENEO YA VIJIJI MIJI SINGIDA, MKANDARASI AKABIDHIWA RASMI MBELE YA DC

 

 Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Muragili (katikati) kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida akiwasha kifaa maalumu cha kupiga king'ora kuashiria uzinduzi rasmi wa mradi mpya wa kusambaza umeme kwenye Vijiji Miji viliyopo pembezoni mwa Manispaa ya Singida katika hafla iliyofanyika Kata ya Mwankoko Desemba 29,2022 ambao utagharimu Sh. 7.11 Bilioni zilizotolewa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) amapo  Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) litakuwa msimamizi wa mradi huo. 

Na Dotto MwaibaleSingida

SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imezindua mradi mpya wa kusambaza umeme kwenye Vijiji Miji viliyopo pembezoni mwa Manispaa ya Singida ambao utagharimu Sh. 7.11 Bilioni na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) litakuwa msimamizi wa mradi huo.

Mradi huo wa kusambaza umeme katika Vijiji Miji (Peri-urban Electrification)  ambao umezinduliwa Desemba 29, 2022 Kitongoji cha Kitope Darajani Kata ya Mwankoko utatekelezwa kwenye vitongoji 34 vilivyopo katika  Kata 9 ambapo wateja watarajiwa ni zaidi ya 2000.

Akizindua Mradi huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Muragili aliwaomba wananchi wachangamkie mradi huo kwa kuanza kuanza kuunganisha nyaya za umeme ili waweze kufungiwa kwa gharama ya Sh.27,000.

"Mradi huu ukikamilika unakwenda kubadilisha uchumi wa wanananchi kwani watautumia umeme huo kuanzisha viwanda vidogo  na shughuli zingine za uzalishaji ambazo zitatumia nishati hiyo hivyo kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla" alisema Muragili.

Muragili alimuomba mkandarasi wa mradi huo kuukamilisha ndani ya mwaka mmoja badala ya miezi 18 aliyopewa  kuukamilisha kwa sababu hakuna sababu yoyote ya kuchelewa kuukamilisha ndani ya muda huo kwa kuwa unatekelezwa kwenye maeneo yenye miundombinu mizuri ya barabara.

Akifafanua kuhusu Mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Nicolaus Moshi  alisema mradi wa usambazaji nishati ya umeme katika maeneo yaliyo pembezoni mwa miji kwa hapa nchini Mkoa wa Singida ndio wanaupata kwa mara ya kwanza.

Alisema mradi huo utajenga jumla ya kilomita 40.5 za msongo wa kati na msongo mdogo na kupitia mradi huo watafunga mashine umba au Transfomer 33 katika vitongoji vilivyotajwa na kuweza kuwaunganishia wateja wa awali 1802 ambapo aliwaomba wananchi wa maeneo utakapo pita mradi huo kuchangamkia fursa hiyo.

Moshi alisema REA imekuwa ikitekeleza miradi mingine mingi hapa nchini Mkoa wa Singida ukiwa ni moja ya mikoa ambayo inanufaika na miradi hiyo na akatumia nafasi hiyo kumtambulisha kwa wananchi na mgeni rasmi Mkandarasi wa Kampuni ya  Central Electricals International Ltd anayetekeleza mradi huo na kukabidhiwa rasmi mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili ili aanze kufanya kazi .

Katika hafla hiyo viongozi mbalimbali walipata fursa ya kutoa salamu huku wakimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huo na mingine mingi na wito wao mkubwa wakiomba wananchi kutunza miundombinu ya mradi huo na kuwataka wachangamkie umeme huo kwa kuanzisha miradi ya kuinua uchumi wao.

Baadhi ya viongozi waliopata fursa ya kutoa salamu ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Singida, Lusia Mwiru, Diwani wa Kata ya Mwankoko, Emmanuel Daniel, Mbunge wa Singida Mjini ambaye aliwakilishwa na Diwani wa Kata ya Kisaki, Moses Ikaku, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwankoko (A) Jacobo Yohana na  Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu.

 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Nicolaus Moshi (kulia) akimkabidhi faili la mkataba wa utekelezaji wa mradi huo, Meneja Mradi wa Kampuni ya Central Electricals International Ltd,  Pravin Thorat inayo jenga mradi huo. Katikati anayeshuhudia tukio hilo ni Mwakilishi wa Mbunge wa Singida Mjini, Diwani wa Kata ya Kisaki, Moses Ikaku.
 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Nicolaus Moshi (kulia) akimkabidhi faili la mkataba wa utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida, Mhandisi Florence Mwakasege.
Picha ya pamoja baada ya kukabidhiana mkataba huo.
 Wafanyakazi wa Kampuni ya Central Electricals International Ltd wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa hafla hiyo.

Wazee wa Kata ya Mwankoko wakiwa kwenye hafla hiyo.ya uzinduzi wa mradi huo.

Post a Comment

Previous Post Next Post