Na Shamimu Nyaki
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.Mohamed Mchengerwa ameiagiza Idara ya Sanaa na Bodi ya Filamu kuhakikisha Mfuko wa Utamaduni na Sanaa unaanza kutoa mikopo kwa Wasanii ifikapo jumatano ya Desemba 21, 2022.
Mhe. Mchengerwa ametoa agizo hilo usiku wa kuamkia Desemba 18, 2022 jijini Arusha katika Usiku wa Tuzo za Filamu mwaka 2022, ambapo amepongeza Wasanii Kwa kuendelea kufanya filamu bora.
" Sekta ya Filamu inakua, na inaendelea kutoa ajira Kwa vijana wengi pamoja na kuchangia katika Pato la Taifa, hivyo sisi kama Serikali tutaendelea kuweka nguvu katika Sekta hiyo" amesema Mhe. Mchengerwa.
Amesisitiza Watendaji wa Wizara kumaliza michakato iliyopo katika utekelezaji wa majukumu kwa wadau wa Sekta za Wizara yake, huku akiwaasa kuweka mazingira rahisi kwa wadau hao kutekeleza majukumu yao.
Katika tukio hilo Mhe. Mchengerwa alipokea Tuzo Maalum kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake katika kukuza Sekta ya Filamu na Kuanzisha Mfuko wa Utamaduni na Sanaa nchini.