RAIS DKT. SAMIA, WAZIRI MCHENGERWA WATUNUKIWA TUZO YA HESHIMA NA SHUKRAN TUZO ZA FILAMU 2022

Na John Mapepele

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa wametunukiwa Tuzo maalum ya shukrani kwa mchango wao katika kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya Sanaa.

Tuzo hizo zimetolewa kwenye kilele cha utoaji wa Tuzo za Filamu 2022 uliofanyika usiku wa kuamkia leo kwenye kituo cha Kimataifa cha Mkutano Arusha, AICC.

Awali kabla ya kukabidhi Tuzo hizo, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Filamu, Dkt. Kiagho Kilonzo amesema Mhe. Mchengerwa amechaguliwa kwa kuzingatia mchango wake mkubwa alioufanya katika kipindi kifupi tangu achaguliwe kusimamia sekta hiyo ambayo inaongoza kwenye kuchangia ukuaji wa uchumi.

Amesema maelekezo ambayo amekuwa akiyatoa na kuyasimamia yamesaidia kukuza Sekta hiyo kwa kiwango kikubwa.

"Ni kutokana na maelekezo thabiti ya Mheshimiwa Waziri ndiyo maana leo tunashuhudia kufanyika kwa mafanikio makubwa utoaji wa Tuzo wa msimu wa pili" amefafanua Kilonzo

Tuzo ya Mhe. Rais ilikabidhiwa na Msanii Nguli Mzee Chilo na kupokewa kwa niaba yake na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa.

Wakati huohuo, Mhe. Mchengerwa ameelekeza Idara ya Sanaa kwa kushirikiana na Bodi ya Filamu kuhakikisha ifikapo jumatano ijayo (siku tano kuanzia kutolewa kwa maelekezo) wasanii wawe wameanza kupata fedha katika Mfuko huo ili waweze kutengeneza kazi nzuri zitakazo pata masoko hatimaye kuboresha maisha yao.

Katika hotuba yake rasmi ya ufunguzi wa utoaji wa Tuzo za Filamu Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuendelea kuwekeza katika kuwasaidia wasanii ili waweze kufanya vizuri.

Akitolea mifano amesema nchi nyingi zilizoendelea kwenye sekta hii zimefanya uwekezaji mkubwa na kueleza kuwa bado kazi kubwa inatakiwa kufanya ili kufika hapo.

Amesisitiza kuwa wasanii wa Tanzania wamekuwa wakifahamika kila sehemu nchini lakini umaarufu wao haulingani na hali halisi ya maisha waliyonayo hivyo kuna haja kubadilika.

 Aidha, ameeleza kuwa Mhe. Mchengerwa anakuwa kiongozi wa pili kupata kupata Tuzo hiyo baada ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliyepata Tuzo kama hiyo kutokana na mchango mkubwa anaoutoa kwenye sekta ya Sanaa katika kipindi chake.

" Mhe Rais Samia tumemtunukia Tuzo hii ya heshima na shukrani kwa mambo makubwa mawili, Kwanza kutenga muda wake kama Rais na kucheza Filamu ya Royal Tour siyo kitu cha kawaida, na pili ni kuturejeshea Mfuko wa Sanaa utakaosaidia wasanii kukopa fedha kwa ajili ya kufanya kazi zao" amefafanua Kilonzo

Katika tukio hilo pia Mkuu wa Mkoa wa Arusha alipewa Tuzo ya shukrani kwa Mkoa kukubali kuwa mwenyeji wa msimu wa pili wa utoaji wa Tuzo za Filamu na kuchangia baadhi ya gharama za shughuli hii.

Msimu wa kwanza uliofanyika mwaka Jana jijini Mbeya.

Jumla ya Tuzo 32 zimetolewa katika msimu huu ambapo kumekuwa na Tuzo maalum zilizotolewa Katika msimu huu ambazo siyo za ushindani katika eneo la Viongozi, wadau na wasanii ambapo mara ya kwanza wasanii 10 waliotoa mchango mkubwa kwenye sekta hii walitunukiwa Tuzo ya TFB fahari.

Wasanii hao ni pamoja na Dr. Sheni, Bishanga, Musa Banzi, Rey, Single Rich, JB, Monalisa, Wema Sepetu, Thecla Mgaya(Aisha) na William Mtitu.

Pia Msanii, Hayati Kanumba amepewa amepewa Tuzo ya Heshima ya mafanikio katika kipindi chote Kwa upande wa wanaume ( lifetime achievement male) na Joyce Mhavile kwa upande wa Wanawake.

Tuzo nyingi za musimu huu zimekwenda kwa wasanii wapya kwenye tasnia zikipokelewa kwa hisia hisia kali huku wasanii wakibubukikwa na machozi ya furaha kutokana na ushindi huu wa kihistoria.

Tukio hilo lilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul na viongozi na wadau mbalimbali wa sanaa huku likipambwa na burudani nzuri kutoka kwa vikundi mbalimbali vya wasanii.

Post a Comment

Previous Post Next Post