Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Desemba 16, 2022, imepatiwa mafunzo ya uongozi na wakufunzi kutoka Chuo Kikuu Mzumbe.
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Chuo Cha Wanyamapori Pasiansi kilichopo jijini Mwanza yamelenga kuongeza ufanisi wa menejimenti katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya kiutendaji.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi, Mabula Misungwi Nyanda amesema mafunzo haya yameandaliwa mahsusi kwa ajili ya kuwajengea uwezo viongozi katika usimamizi wa masuala mbalimbali ikiwemo rasilimali watu, fedha na taratibu za manunuzi.
" Ni matumaini yangu kuwa baada ya mafunzo haya kutakuwa na mabadiliko ya utendaji katika maeneo mnayosimamia" amesema Kamishna Mabula.
Mafunzo haya ya uongozi yametolewa kwa Manaibu Kamishna, Makamanda wa Kanda, Makamishna Wasaidizi Wandamizi na Makamishna Wasaidizi.