TANZANIA YAKAMILISHA MKAKATI WA KITAIFA WA KUREJESHA MANDHARI YA MISITU

 

Tanzania imekamilisha maandalizi ya Mkakati wa Kitaifa wa Kurejesha Mandhari ya Misitu wenye lengo la kuongoa ardhi iliyoharibika kutokana na shughuli za kibinadamu.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii leo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Donge, Mhe. Mohamed Soud aliyetaka kujua Kampeni ya AFR imetekelezwa kwa kiasi gani.

Amesema mkakati huo unatarajiwa kuwasilishwa katika Mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa kujadili masuala ya Mazingira unaotarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 30,2022 nchini Misri.

Sambamba na hilo amesema Serikali imesaini makubaliano ya Kurejesha Mandhari ya Kiafrika- kupitia kampeni ya AFR 100 iliyokuwa na adhma ya kuongoa hekta milioni 100 za ardhi iliyoharibiwa barani Afrika.

Kupitia kampeni hiyo Tanzania iliahidi kuongoa hekta milioni 5.2 za ardhi iliyoharibiwa ambapo kwa sasa inatekelezwa kwa Kuondoa wavamizi na kurejesha ardhi iliyoathiriwa, kuimarisha usimamizi wa misitu ya mikoko, kutoa elimu ya kudhibiti moto wa msituni ili kulinda uoto wa asili na kutekeleza Mpango wa Dodoma ya Kijani.

Awali, akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Antropia Theonist kuhusu waathirika wa wanyama wakali katika Wilaya ya Kyerwa, Mhe. Masanja ametoa pole kwa wananchi walioathirika na wanyama hao na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kufanyia kazi suala la kifuta jasho/machozi.

Post a Comment

Previous Post Next Post