TANZANIA MWENYEJI MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA MKATABA UNESCO

 Na Jane Edward, Arusha


Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano mkubwa wa Kimataifa unaohusiana na mkataba wa usimamizi wa maeneo yaliyo katika orodha ya urithi wa dunia inayotambuliwa na shirika la umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Sayansi,elimu na utamaduni (UNESCO).

Maadhimisho hayo ya miaka 50 ya mkataba UNESCO wa urithi wa kidunia wa asili na kitamaduni, ulioletwa mwaka 1972 na kuridhiwa na Tanzania mwaka 1977, maadhimisho yanayotarajiwa kufanyika Disemba 12 hadi 14, 2022.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha katika semina ya kuelimisha wanahabari juu ya mkataba huo mkuu wa kitengo cha sayansi asilia kutoka shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia masuala ya sayansi, elimu na utamaduni (UNESCO) Kevin Robert alisema maadhimisho hayo yataenda sambamba na mkutano unaolenga kuipa UNESCO, nchi wanachama pamoja na wadau kuweza kuangalia na kujadili mafanikio ya mkataba, changamoto zinazowakabili nchi wanachama pamoja na kijifunza utekelezaji wa mkataba huo .

“Tanzania imepewa jukumu la kuandaa mkutano huu kwasababu ni mwanachama wa UNESCO lakini pia ni miongoni mwa nchi za mwanzo kuridhia mkataba huu pamoja na kuwa na historia nzuri ya kutekeleza mkataba huu toka 1977 na kufanya kuwa nchi ya mfano kwaajili ya kijifunza ikiwa ni pamoja na kuweza kutatua changamoto zinazo tokea katika maeneo haya kwa njia ya maridhiano,” Alisema Kevin Robert.

Aidha pamoja na kuwa Tanzania ni mojawapo ya nchi wanachama zilizopo katika utekelezaji mzuri wenye mafanikio pia ina maeneo saba yaliyopo kwenye orodha ya urithi wa kidunia huku maeneo mengine saba yakiwa katika hatua ya kusubiri kuingizwa katika orodha hiyo.

“Maeneo yaliyotambulika na UNESCO kama urithi wa kidunia wa kitamaduni hapa Tanzania ni pamoja na Stone Town -Zanzibar, Kilwa kisiwani na Kondoa rock art, na ya asili ni Kilimanjaro, Serengeti na Selous pamoja na eneo Ngorongoro ambalo ni la urithi mchanganyiko wa kimazingira na binadamu,” Alisema Keven Robert.

“Maeneo saba mengine hapa nchini yanayosubiri kuingia kwenye orodha ya urithi wa kidunia ni Oldonyo Morwak, Gombe, Jozani, chwaka bay conservation area, Eastern arc mountains, central slave na ivory trade route,” Alibainisha.

Alifafanua kuwa lengo la mkataba huo ni kuleta uhalali wa orodha ya kidunia katika usawa wa kimazingira na kitamaduni, kuwa na hifadhi sahihi ya maeneo hayo, kutangaza na kujenga uwezo wa kupata misaada, kutoa elimu na uelewa juu ya umuhimu wa kuwa na maeneo hayo pamoja na ushiriki wa jamii katika urithi huo katika usimamizi na utekelezaji wa mkataba huo.

Kwa Upande wake Kamishna msaidizi mwandamizi wa uhifadhi kotoka mamlaka ya hifadhi Ngorongoro, Mhandisi Joshua Mwankonda alisema semina hiyo ni muendelezo wa namna ambayo mamlaka hiyo inatoa elimu kwa ukubwa wake wa uhifadhi, maendeleo pamoja na utalii kwa wanahabari ambapo kutokana na maadhisho hayo na mkutano huo wameona ni vema kutoa elimu juu ya mkataba huo wa uridhi wa kidunia ambapo elimu yake na taarifa zake bado zipo chini.

“Ni kuongeza uelewa wa nini maana ya mkataba huo ambao nchi yetu imeridhia na nini katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro kinafanyika katika huu mkataba na kwasasa imekuwa ni agenda kitaifa na kimataifa, kupata wataalamu wengi wa kiafrika ambao watakuwa wanafanya shughuli hizi tofauti na miaka ya nyuma ambayo ilikuwa inaoneka ilikuwa inafanywa na wazungu pekee katika maeneo ya hifadhi na kusimamia mkataba huu na kuhifadhi wa urithi huu kwa kizazi hiki na kizazi kijacho kwa faida za kielimu sayansi na utalii,”Mhandisi Mwankonda.

Hata hivyo zaidi ya wataalamu 50 kutoka nchi mbalimbali Duniani wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo utakaoenda sambamba na maadhisho hayo ambapo Afrika Ina urithi wa kidunia wa asili na kitamaduni 98 sawa na asilimia 8.5, nchi za Uarabuni zikiwa zinazo 88 sawa na asilimia 7.6, Asia na Pacific 277 sawa na asilimia 24.0, Europe na north America 545 sawa na asilimia 47.2, pamoja na Latin America na Caribbean146 sawa na asilimia 12.7 jumla dunia nzima zikiwa ni 1154 huku maeneo mengine katika nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Tanzania yakisubiri kuingia katika orodha hiyo.

Kamishna msaidizi mwandamizi wa uhifadhi kutoka mamlaka ya hifadhi  Ngorongoro, Mhandisi Joshua Mwankonda akifafanua jambo kwa waandishi wa habari
Mkuu wa kitengo cha sayansi asilia kutoka shirika la UNESCO Kevin Robert akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha.

Post a Comment

Previous Post Next Post