Na Muhidin Amri, Kilolo
WANANCHI wa kijiji cha Kimala wilaya ya Kilolo mkoani Iringa,wameishukuru Serikali kupitia wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kwa kutimiza ahadi ya kuwajengea mradi wa maji ambao umefanikisha kumaliza kero ya huduma hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema,tatizo la maji katika kijiji cha Kimala kilichopo mpakani mwa Mikoa ya Iringa na Morogoro ni la miaka mingi na limesababisha wananchi hao kukosa muda wa kufanya shughuli za uzalishaji mali kwa kuwa wanatumia muda mwingi kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku.
Wamesema hayo mbele ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Mhandisi Clement Kivegalo, aliyetembelea mradi wa maji katika kijiji hicho unaotekelezwa na Ruwasa kwa gharama ya Sh.milioni 561,490,936,576.50.
Sadia Kiwele alisema,wananchi wa kijiji hicho ni waathirika wakubwa wa tatizo la maji kwani walilazimika tokana kutumia kati ya masaa 2 na 3 kwenda kutafuta huduma hiyo muda ambao wangeweza kuutumia katika shughuli mbalimbali za kujipatia kipato.
Hata hivyo,ameishukuru serikali ya awamu ya sita kupitia Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa),kwa kutekeleza mradi huo mzuri ambao umemaliza changamoto ya huduma ya maji katika kijiji hicho.
Mwananchi mwingine wa kijiji hicho Jack Kikoti alisema, kukamilika kwa mradi huo ni faraja kubwa kwa wananchi wengi ambapo sasa wanapata muda mwingi wa kujikita katika shughuli za uzalishaji mali tofauti na hapo awali.
Aidha alieleza kuwa,ukosefu wa maji safi na salama katika kijiji hicho umesababisha hata baadhi ya ndoa kuvunjika pale wanawake wanapotumia muda mwingi kwenda kutafuta maji kwenye vyanzo vya asili ambavyo havikutosheleza mahitaji yao.
Kiwele,ameiomba Ruwasa wilaya ya Kilolo kupeleka miundombinu ya maji kwenye maeneo ya pembezoni ambayo bado hayajafikiwa na huduma hiyo ili wananchi wa maeneo hayo waweze kufaidi matunda ya Serikali.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Clement Kivegalo amewapongeza wananchi hao kwa kupata mradi mzuri wa maji, lakini amewataka kuwa walinzi wa miundombinu na kuutunza vizuri mradi huo ili uweze kutoa huduma kwa muda mrefu.
“katika ziara yetu tumeanzia mkoa wa Ruvuma na Njombe na sasa tumekuja Iringa,hata hivyo kuna baadhi ya miradi tuliyoikuta hatukulidhika sana kwenye ujenzi wa miundombinu yake,kwa hiyo nawapongeza sana wananchi wa kijiji cha Kimala kupata mradi mzuri”alisema Kivegalo.
Kwa mujibu wa Mhandisi Kivegalo,serikali kupitia Ruwasa inaendelea kuwekeza fedha na kujenga miradi ya maji ili huduma hiyo iweze kuwafikia wananchi wengi katika vijiji mbalimbali hapa nchini.
Alisema,ni wajibu wao kumaliza tatizo la maji kwa wananchi ambapo wamejipanga kufikia lengo la asilimia 85 maeneo ya vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo mwaka 2025 kwa kutekeleza miradi ya maji kwenye meneo yasiyokuwa na huduma hiyo.
Aidha Kivegalo,amewataka wananchi wa kijiji hicho na vijiji vingine ambavyo Ruwasa inatekeleza ujenzi wa miradi ya maji,kuchangia huduma ili miradi hiyo iwe endelevu badala ya kurudi walikotoka kwa kutumia vyanzo visivyo rasmi.
Katika hatua nyingine Kivegalo, amempongeza Meneja wa Ruwasa mkoa wa Iringa Joyce Bahati kwa kutekeleza na kusimamia vizuri miradi ya maji iliyojengwa na inayoendelea kujengwa katika mkoa huo.
Alisema,katika mkoa wa Iringa miradi mingi ya maji imejengwa kwa viwango na ubora wa hali ya juu,na kuwaomba wananchi kuhakikisha wanatunza miundombinu na miradi hiyo kwa manufaa yao.
Naye Mkurugenzi wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira kutoka Wizara ya Maji CPA Joyce Msiru,amewaasa wananchi wa Kimala kuepuka uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji ili miradi inayojengwa iweze kudumu na kutoa huduma endelevu.
Awali Meneja wa Ruwasa wilayani Kilolo Enock Basyagile alieleza kuwa,ujenzi wa mradi mpya wa maji ya mserereko katika kijiji cha Kimala ulianza kutekelezwa mwezi Februari 2022 na unatarajiwa kukamilika mwezi Februari mwakani.
Alisema,mradi huo umesanifiwa kuhudumia jumla ya wakazi 2,800 wa kijiji hicho na gharama za ujenzi ni Sh.milioni 561,490,794.38 ambapo fedha iliyolipwa kwa mkandarasi ni Sh.milioni 264,936,576.51 ikiwa ni malipo ya hati na malipo ya awali.