Na. Catherine Mbena/TANAPA
Kamishna wa Uhifadhi, William Mwakilema wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), amewataka makamishna wapya kufanya kazi kwa weledi, ushirikiano na kufuata taratibu katika kutekeleza majukumu yao mapya.
Kamishna Mwakilema ameyasema hayo leo katika Makao Makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania jijini, Arusha wakati wa zoezi la kuwavisha vyeo na kuwaapisha makamishna wateule wa Uhifadhi walioteuliwa na Bodi ya Wadhamini ya shirika hilo kushika nafasi mbalimbali za uongozi.
“Uongozi ni dhamana, na unapokuwa kiongozi unatarajiwa kuwa dira kwa wale unaowaongoza kwa namna zote. Wafuasi wako wataangalia Mienendo yako, kauli zako, na matendo yako hivyo kiongozi unatakiwa kuwa mfano wa kuigwa.” Alisema Mwakilema.
Aidha, Kamishna Mwakilema amewaasa makamishna wapya kuwa na uongozi shirikishi ili yale maamuzi watakayoyafanya yawe ya pamoja ili kuleta tija katika maeneo ya kazi.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi Herman Batiho -Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara, aliwaasa makamishna hao kutenda haki kwa watumishi wanao kwenda kuwaongoza na kubainisha ni matarajio ya uongozi wa TANAPA kuona changamoto zote katika maeneo ya kazi zinatatuliwa.
Hivi karibuni Bodi ya Wadhamini ya TANAPA ilifanya uteuzi katika nafasi mbalimbali za uongozi pamoja na kuwapandishwaji vyeo wa viongozi waandamizi wa shirika kwa lengo la kuboresha utendaji kazi ambapo ilimpandisha cheo Afisa Uhifadhi Mkuu Mackiyu Kajwangya, kuwa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na kiongozi wa Marubani wa Shirika.
Afisa Uhifadhi Mkuu, Richard Kafwita kuwa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Idara ya Menejimenti ya Rasilimali Watu.
Afisa Uhifadhi Mkuu, Yustina Kiwango kuwa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Arusha.
Na Afisa Uhifadhi Mkuu, Charles kuwa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na kuwa Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Rumanyika-Karagwe.