BARAZA LA WAFANYAKAZI LATAKIWA KUSIMAMIA UTENDAJI KAZI, NIDHAMU

 






 Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa, amewataka wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kuhakikisha kuwa wanasimamia ipasavyo  utendaji kazi pamoja na nidhamu ya watumishi ili kuongeza ufanisi wa Taasisi.

Bw. Nyaisa ametoa agizo hilo leo tarehe 11 Novemba, 2022 wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza  la Wafanyakazi  kinachofanyika mkoani Morogoro.

Bw. Nyaisa amesema kwakuwa Baraza la Wafanyakazi ni chombo cha ushirikishaji wa watumishi na linaundwa na wajumbe kutoka Menejimenti ya BRELA, viongozi wa Chama cha Wafanyakazi (TUGHE)  na wawakilishi wa watumishi kutoka idara mbalimbali, wajumbe wote wanao wajibu wa kusimamia utendaji kazi pamoja na nidhamu ya watumishi ili kutoharibu taswira ya Taasisi.

Bw. Nyaisa amesema pia  viongozi wa  TUGHE kama wajumbe wa Baraza wanapaswa kufuatilia maslahi ya wafanyakazi kwa kushirikiana na Menejimenti, hivyo  wanapoona  kuna jambo lolote ambalo haliendi sawa wanapaswa kutoa taarifa mapema. 

"Siyo jambo jema kwa viongozi wa TUGHE kukaa kimya kwa mambo ambayo yako wazi na kusubiri Menejimenti ya Taasisi ndiyo afuatilie,"amesisitiza Bw. Nyaisa.

Akizungumzia umuhimu wa Vikao vya Baraza Bw. Nyaisa amesema, vikao vinasaidia  kutatua changamoto za wafanyakazi kwa uwazi na kuondoa manung'uniko ambayo yanaweza kujitokeza.

Pamoja na mambo mengine Baraza la wafanyakazi hukutana mara 2 kila mwaka, kuidhinisha mipango na bajeti ya wakala pamoja na kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa malengo ya wakala kwa mwaka

Post a Comment

Previous Post Next Post