KUNDI LA 15 KUTOKA NGORONGORO LAHAMIA MSOMERA

 Na Kassim Nyaki, NCAA 

Kundi la 15 la wananchi wanaohama kwa hiari kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera limeondoka leo tarehe 08 Novemba, 2022 baada ya kuagwa na mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Raymond Mangwala.

Kwa mujibu wa Naibu Kamishna wa Uhifadhi NCAA, Needpeace Wambuya, Wananchi wanaohama katika awamu hii wanajumuisha kaya 50 zenye wananchi 317 pamoja na Mifugo 1,604.

Naibu Kamishna Wambuya ameeleza kuwa zoezi la kuhamisha wananchi waliojiandikisha kuhama kwa hiari kwenda Kijiji cha Msomera ambalo lililoanza mwenzi juni, 2022 hadi tarehe 08 Novemba, 2022 linapoagwa kundi la 15, Jumla ya kaya 457 zenye watu 2,442 na mifugo 13,094 zimeshahamia Kijiji cha Msomera kwa ajili ya kupisha shughuli za Uhifadhi katika eneo la Ngorongoro.

Amebeinisha kuwa wananchi katika Tarafa ya Ngorongoro wameendelea kujiandikisha kwa wingi kupisha shughuli za Uhifadhi na Serikali kupitia NCAA itaendelea kuwahamisha kwa awamu kadri inavyoboresha mazingira na huduma muhimu za kijamii maeneo wanayohamia.

Akiwaaga wananchi hao Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Raymond Mangwala amesema

 “Msomera mnakohamia mtafurahia maisha na hamtajutia, Serikali imeweka mazingira wezeshi na mtapata huduma zote za kijamii ikiwemo Shule, maji, barabara, mawasiliano, vituo vya afya, umeme, maeneo ya malisho, malambo na majosho kwa kwa ajili ya mifugo yenu na Serikali itaendelea kuboresha huduma hizo kadri wananchi wanavyojiandikisha kuhamia kuhama kwa hiari”

Mhe. Mangwala ameongeza kuwa kundelea kujitokeza kwa wanchi wengi ni ishara njema katika kustawisha uhifadhi na ikolojia ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuwa shughuli nyingi za kibinadamu zinapungua na wananchi nao wananufaika na upatikanaji wa huduma bora nje ya Hifadhi tofauti wanapokuwa ndani ya Hifadhi. 

“Kadri wananchi wanavyojitokeza kuhama ndani ya Hifadhi ndio inasaidia mazingira ya hifadhi kuwa tulivu na kuongeza uoto wa asili hivyo tunaamini shughuli za Uhifadhi, utalii na ikolojia ya mazingira kwa ujumla unaendelea kushamiri kutokana na kupungua kwa shughuli za binadamu.

Bi. Siteya Melubo Mollel ambaye ni mke wa Mbunge mstaafu wa Ngorongoro marehemu William Ole Nasha amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kusaidia wananchi wa Ngorongoro kuhama kwa hiari na kuwaandalia makazi mazuri ambaayo ni bora kuliko walikotoka.

Ameongeza kuwa wananchi wanaohamia Msomera wamepata fursa ya kwenda kujenga nyumba za kudumu, kufanya biashara kwa uhuru tofauti na waalivyokuwa ndani ya Hifadhi.

“Sisi akina mama na Watoto huu ni msaada mkubwa wa kupata makazi salama na huduma muhimu ambazo ni mahitaji ya binadamu, wengine waliobaki kwenye hifadhi waichukulie hii kama fursa ya kuboresha maisha yao binafsi na hatma njema ya Watoto wao hapo kwa miaka ijayo” ameongeza Siteiya Mollel.

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Raymond Magwala akimkabidhi hundi ya Malipo Bibi Siteiya Mollel ambayo ni moja ya wananchi walioamua kuhama kwa hiari katika Hifadhi ya Ngorongoro, Katikati ni Naibu Kamishna, Needpeace Wambuya-Huduma za Shirika NCAA


Wananchi wanaohamia Kijiji cha Msomera wakiagwa




Post a Comment

Previous Post Next Post