Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo,Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa usiku wa kuamkia leo Julai 29 ameshiriki uzinduzi rasmi wa mashindano ya Jumuiya ya Madola nchini Uingereza.
Ufunguzi huo wa mashindano ya mwaka huu yamefana huku wageni kutoka nchi mbalimbali duniani za Jumuiya ya Madola wakiwa wameshiriki.
Timu ya wanamichezo inayoshiriki mashindano haya kutoka Tanzania nayo iliingia katika uwanja wa michezo huku ikiwa na hamasa. nyingine na kushangiliwa na maelfu ya watazamaji.
Katika tukio hilo Mhe. Mchengerwa akiambatana na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Dkt, Asha Rose Migiro, Mhe. Musa Sima (Mb) na Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na Naibu Katibu Mkuu. Saidi Yakubu alipata fursa ya kubadishana mawazo na viongozi kutoka nchi mbalimbali duniani kwenye maeneo ya sekta ya Michezo.
Mhe. Mchengerwa amesema kuwa Tanzania imejifunza mambo mengi kwenye mashindano haya ambapo amesisitiza kuwa baada ya kurejea nyumbani kutafanyika maboresho makubwa.
Aidha, amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuhakikisha kuwa michezo inaendelezwa ili kutoa ajira na kuchangia kwenye uchumi wa taifa.
Amesema kwa sasa Serikali inakwenda kutekeleza mkakati wa kusaka vipaji vya michezo wa mtaa kwa mtaa.
Naye Mhe.Sima amesema kuwa michezo iwe fursa ya kuimarisha diplomasia na nchi nyingine.