Na John Mapepele, London
Balozi wa Tanzania, nchini Uingereza. Dkt, Asha Rose Migiro amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa jicho la pekee kwenye sekta ya michezo.
Mhe Balozi Migiro ametoa kauli hiyo leo Julai 29, 2022 nchini Uingereza kwenye mashindano ya Michezo ya Jumuiya ya Madola ambapo Tanzania inashiriki.
"Hapa napenda kusema kwa dhati kama Balozi mwanamke wa Tanzania hapa Uingereza kuwa namshukuru Mhe. Rais kwa kutoa kipaombele kwenye michezo na sasa tunaona mafanikio makubwa kwenye michezo ya wanawake' ameongeza Mhe. Migiro
Hadi sasa tayari timu ya taifa ya soka ya wanawake chini ya umri wa miaka 17 ( Serengeti Girls) na timu ya taifa ya wanawake ya Kabbadi zimefuzu kuingia kwenye mashindano ya dunia ya michezo hiyo.
Aidha, amempongeza wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kazi nzuri inayofanya ya kuitangaza Tanzania duniani kupitia michezo.
Akizungumzia kuhusu ushiriki wa Tanzania kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola amesema anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwa mwaminifu kwenye Jumuiya.
"Tunaishukuru pia wizara tumekuwa na ushirikiano na umechangia umadhubuti wa mashindano" amefafanua Mhe. Migiro
Pia amesema ushiriki wa Tanzania kwenye mkutano wa 10 wa Mawaziri wa Michezo wa nchi za Jumuiya za madola umekuwa na umuhimu kwa vile ndiyo mkutano unaotengeneza Sera na mipango mbalimbali.
Katika mkutano huo mambo kadhaa yamejadiliwa ikiwa ni pamoja na haki za binadamu na umuhimu wa kuheshim na kulinda utu wa wanamichezo
Pia mbinu mbalimbali za kuwekeza kwenye michezo.