NAIBU WAZIRI WA MALIASILI AFANYA ZIARA YA KIKAZI MAKAO MAKUU YA TAWA

 



NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Mary Masanja (Mb) leo Julai 29, 2022 ametembelea ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) zilizopo mkoani Morogoro.

Ziara hiyo imelenga kuzungumza na menejimenti na watumishi wa TAWA kuhusu masuala mbalimbali yanayoihusu Mamlaka, ikiwa ni muendelezo wa ziara zake katika Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Masanja ameipongeza TAWA kwa kazi nzuri ya usimamizi wa rasilimali za wanyamapori nchini, licha ya kuwa ni Taasisi changa kuliko zote zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

"Pamoja na uchanga na uchache wenu kwenye Wizara mmeweza kushikamana vizuri , mmepokea majukumu yenu na mnafanya kazi nzuri usiku na mchana", amesema.

Sambamba na hilo, Mhe. Masanja amesisitiza nidhamu na uadilifu kwa watumishi wote na kuwataka wahifadhi kuzifuata na kuziishi kanuni za Jeshi la Uhifadhi.

"Tufanye kazi kwa uadilifu tukiziangalia kanuni zetu za Jeshi la Uhifadhi, wale wachache wanaopaka madoa Jeshi letu tuwaepuke na ikiwezekana tuwaripoti", amesisitiza.

Katika ziara hiyo Mhe. Masanja ameiagiza TAWA kuongeza kasi ya utekelezaji wa mikakati ya kudhibiti wanyama wakali na waharibifu ikiwemo, zoezi endelevu la utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu namna bora ya kujilinda na wanyamapori wakali na kuongeza kasi ya ujenzi wa vituo vidogo vya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa TAWA, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi Mabula Misungwi Nyanda, amezungumzia masuala mbalimbali yakiwemo majukumu ya TAWA, mafanikio na changamoto mbalimbali zinazoikabili Mamlaka ikiwemo suala mtambuka linalohusu wanyamapori wakali na waharibifu.

Vilevile Kamishna Mabula amemshukuru Mhe. Masanja kwa kutenga muda wake kuitembelea TAWA na kuahidi kutekeleza maagizo yote aliyoyatoa.


Post a Comment

Previous Post Next Post